Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Wanaushirika mkoani Iringa wametakiwa kulipa madeni kwa wakati ili kuepuka riba kubwa inayotokana na kuchelewa kulipa mkopo kutoka taasisi za kifedha.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua jukwaa la ushirika mkoa wa Iringa lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa hivi karibuni.
Masenza alisema kuwa wanaushirika wamenufaika na mikopo inayotolewa na taasisi mbalimbali mkoani Iringa. Alisema kuwa pamoja na manufaa hayo, changamoto kubwa imebaki kurejesha mikopo hiyo kwa wakati. Aliwaasa wanaushirika kulipa kwa muda mikopo wanayokopeshwa. “Nawaasa wanaushirika wenye mikopo kulipa madeni yao kwa wakati ili kuepukana na riba inayoendela kupanda. Tukifanya hivyo tutasaidia kujua hali ya uzalishaji hivyo kuvutia wanunuzi wengi zaidi katika Mkoa wetu” alisema Masenza.
Akiongelea sekta ya ushirika katika maendeleo ya wananchi, mkuu wa mkoa alisema kuwa ushirika ni nguzo muhimu katika kuwasaidia wananchi kupata huduma za ushirika kwa urahisi na gharama nafuu. “Mwaka huu vyama vya ushirika vya kilimo sita vimepata mikopo ya pembejeo toka benki ya maendeleo ya kilimo wenye thamani ya Tsh. 277,905,600/= kwa lengo la kuendeleza Kilimo kwenye maeneo yao kupitia udhamini wa chama kikuu cha ushirika -IFCU (1993) LTD. Napenda kutoa wito kwa vyama hivyo vilivyopata mikopo ya kilimo kukusanya mazao yao kwa pamoja katika maghala ili waweze kuuza kwa pamoja na kupata soko zuri” alisema Masenza.
Jukwaa la ushirika mkoa wa Iringa ni la pili na lilihudhuriwa na Katibu Tawala Mkoa, wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa, taasisi za fedha na wanaushirika.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.