Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini mkoani Iringa wametakiwa kuzingatia suala la lishe wakati wanawake wanapokuwa wajawazito na wanapojifungua ili kuwa na watoto wenye hali nzuri ya lishe.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akiongea na wanufaika wa mpango wa TASAF na kamati ya usimamizi ngazi ya jamii alipotembelea wanufaika wa elimu wa mpango wa TASAF katika Kata ya Kitwiru Manispaa ya Iringa hivi karibuni.
Ayubu aliitaka kamati ya usimamizi ngazi ya jamii na serikali ya kijiji kuwasisitiza wanufaika waa TASAF wanapokuwa wajawazito kuhudhuria vituo vya afya ili kupewa elimu ya lishe. Alisema kuwa elimu ya lishe ni muhimu kwa makuzi ya mtoto tokea akiwa tumboni kwa mama yake. “Siku 1,000 ni muhimu sana kwa lishe katika mchango wa makuzi ya mtoto. Ukosefu wa lishe husababisha kutokuwa vizuri na kudumaa kiakili” alisema Ayubu. Alisema kuwa hali hiyo isipoangaliwa mapema inasababisha mzunguko wa umasikini katika familia na jamii kwa ujumla. Aliwasisitiza wanufaika wa fedha za kliniki kuhudhuria kliniki kwa sababu serikali imekopa fedha ili kunusuru wananchi wake katika suala la lishe.
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa alifanya ziara maalum ya ufuatiliaji kwa wanafunzi wanufaika wa mpango wa TASAF kupitia elimu katika Manispaa ya Iringa kujifunza changamoto zinazowakabili. Katika ziara hiyo aliambatana na mratibu wa TASAF Mkoa, afisa mipango, mhasibu, mkaguzi wa ndani na afisa habari.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.