Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Watoto wanaoishi katika mazingira magumu wametakiwa kusoma kwa bidii ili wawe kielelezo kwa watoto wengine nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipoongoza kikundi cha kina mama cha Utulivu kutembelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu wanaolelewa na kituo cha Dar Bilal na kuwapa zawadi za sikukuu ya Idi El Fitri mjini Iringa.
Masenza alisema kuwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu hawajatengwa na jamii. Serikali inawatambua na itaendelea kusimamia ustawi wao ili waweze kukua na kupata elimu kama watoto wengine. Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli imeanzisha mpango wa elimu msingi bila malipo ili watoto wote wa kitanzania waweze kunufaika na elimu hiyo, alisema. “Elimu dunia ni muhimu sana kwa watoto katika kufanikisha juhudi za serikali za kuhakikisha kila mtoto anapata elimu nchini na kutoa mchango wake katika maendeleo ya taifa” alisema Masenza.
Awali mwenyekiti wa kikundi cha kina mama cha Utulivu, Sada Hassan alisema wakina mama wanawajibu wa kuwa karibu na watoto sababu wao ndiyo wazazi. Kina mama wanawajibu wa kuwalea na kuwalinda watoto pasipo kujali changamoto zinazojitokeza katika maisha yao, aliongeza.
Nae msimamizi wa makao ya watoto ya Dar Bilal, Ally Hassan alisema kuwa makao hayo yanakabiliwa na changamoto ya vifaa vya shule. Alitoa wito kwa jamii kujenga utamaduni wa kuwajali watoto wanaishi katika mazingira hatarishi na makao ya watoto ili waweze kufikia ndoto zao. “Jukumu la malezi kwa watoto wanaoishi katika makao ya watoto si jukumu la wasimamizi wa vituo pekee, bali ni jukumu la jamii nzima” alisema Hassan.
Akimkaribisha mkuu wa Mkoa wa Iringa, Afisa Wanyamapori katika ofisi ya mkuu wa Mkoa, Hawa Mwechaga alisema kuwa ziara hiyo itatembelea vituo viwili ambayo ni makao ya watoto walio katika mazingira hatarishi. Alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kuonesha upendo, mshikamano na kuwafariji watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi katika majira haya kuelekea sikukuu ya Idi El Fitri. Alisema kuwa zawadi zilizotolewa kwa watoto ni unga, sabuni, mbuzi, mchele, nguo za ndani biscut, pipi, madaftari, peni na nguo kwa ajili ya walezi vyote vikiwa na thamani ya shilingi 1,390,000.
Makao ya watoto ya Dar Bilal yaliyopo eneo la Ilala Manispaa ya Iringa yana watoto 115, kati yao wavulana 55 na wasichana 60.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.