Makamu Mwenyekiti tume huru ya Taifa ya uchaguzi, Jaji (R) (MST) Mbarouk S. Mbarouk amesema kuwa watu wenye mahitaji maalumu watapewa kipaumbele cha kujiandikisha bila ya kulazimika kusubiri kupanga foleni.
Mhe. Mbarouk ameyasema hayo Disemba 15, 2024 Wakati akifungua mkutano wa tume na Wadau wa uchaguzi kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa uliyopo kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wenye kauli mbiu ya inayosema "Kujiandikishia kuwa mpiga kura ni msingi wa uchaguzi bora".
Akizungumza katika ufunguzi huo Mhe. Mbarouk amefafanua kwamba hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa haki za watu wenye ulemavu, wazee, na makundi mengine yenye mahitaji maalumu zinaheshimiwa na kutekelezwa kwa usawa hivyo mchakato wa kujiandikisha katika daftari la kudumu utaendelea kuwa rahisi kwa watu hao ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi bila vikwazo vya aina yoyote.
"Ni muhimu kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anapata fursa ya kushiriki katika uchaguzi bila kujali changamoto anazokutana nazo, Kwa hiyo watu wenye mahitaji maalumu watapewa kipaumbele maalumu katika vituo vya kujiandikisha ili wasiwekewe vikwazo vya aina yoyote na hakuna mtu atakayezuiliwa kutokana na hali yake ya kiafya au kimwili", amesema Mbarouk
Pia ameongeza kwa kusema kuwa Tume ya Uchaguzi itahakikisha kuwa vituo vya kujiandikisha vitakuwa na mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa vifaa na msaada wa ziada ili kuwasaidia katika mchakato huo na kuongeza kwa kutoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano na kuhamasisha watu wenye mahitaji maalumu kujitokeza na kujiandikisha ili waweze kutumia haki yao ya kupiga kura katika uchaguzi ujao.
Mkutano huo uliofanyika Mkoani Iringa ni sehemu ya jitihada za Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika kuelimisha na kuwashirikisha wadau wa uchaguzi kuhusu umuhimu wa kujiandikisha kama wapiga kura na umuhimu wa kuwa na daftari la mpiga kura.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.