Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Benki ya MUCOBA imepanga kutoa mikopo ya kilimo zaidi ya shilingi bilioni tano katika kuunga mkono juhudi za Rais Dkt John Magufuli za kuendeleza sekta ya kilimo nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na meneja mkuu wa benki ya MUCOBA, Ben Mahenge alipokuwa akisoma taarifa ya benki hiyo katika hafla ya uzinduzi wa mfumo wa stakabadhi ghalani katika Tarafa ya Pawaga wilayani Iringa.
Mahenge alisema “mheshimiwa mgeni rasmi, kwa mwaka 2018 benki imepanga kutoa mikopo ya kilimo yenye thamani ya shilingi bilioni 5.052”. Alisema kuwa lengo ni kuwawezesha wakulima kuzalisha kwa wingi, na kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Magufuli ya kuongeza kipato kwa wakulima. Mwaka jana benki ilianzisha mikopo inayoitwa wakulima Digital kwa ushirikiano wa AGRA na SELF, alisema. Mikopo hiyo hutolewa kwa awamu tatu kwa mkulima. Alizitaja awamu hizo kuwa ni wakati wa maandalizi ya shamba, wakati wa kilimo na kupalilia na wakati wa kuvuna.
Akiongelea faida za mikopo hiyo, alizitaja kuwa ni kupunguza usumbufu na muda wa kupata mkopo, kupunguza gharama za kufuata mkopo kwenye vituo na kutunza siri za wateja. Faida nyingine alizitaja kuwa ni usalama wa wateja kuimarishwa na kupunguza matumizi yasiyo lengwa.
Meneja huyo alisema kuwa benki yake iliona ni jambo jema kutoa mikopo ya stakabadhi ghalani hasa kipindi cha mavuno. Lengo ni kuwawezesha wakulima kuweza kupata fedha ya kuvunia na kujikimu katika kipindi ambacho watakapo kuwa wametunza mazao yao ghalani wakisubirishia bei ya mazao yao kuongezeka sokoni ili waweze kuuza kwa bei nzuri, alisema.
Akiongelea changamoto ya dhamana kwa wakulima, alisema kuwa wakulima wengi hawana dhamana na kusema kuwa dhamana ya wakulima itakuwa mazao yao yatakayokuwa yametunzwa gharani.
Ikumbukwe kuwa benki ya MUCOBA imejikita kuwahudumia wananchi wa kipato cha chini hasa wakulima ikiwa imetoa mikopo ya kilimo kiasi cha shilingi bilioni 11 kwa mwaka 2015, 2016 na 2017.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.