Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wilaya ya Kilolo imetoa wito kwa wanafunzi wanaosoma chuo cha Taifa cha ulinzi kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo wilayani Kilolo kwa lengo la kujifunza na kuburudika.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah alipokuwa kiongea na ujumbe wa wanafunzi kutoka chuo cha Taifa cha ulinzi waliotembelea kiwanda cha Dabaga kwa lengo la kujifunza sekta ya viwanda inavyofanya kazi wilayani Kilolo.
Abdalla alisema kuwa timu ya wanafunzi kutoka chuo cha Taifa cha ulinzi wapange kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo wilayani Kilolo. Alisema kuwa wilaya hiyo inavyo vivutio vya aina tofauti ikilinganishwa na maeneo mengine. Alisema kuwa Wilaya ya Kilolo wanapatikana Mbega wekundu ambao hawapatikani sehemu nyingine.
Alisema kuwa pamoja na mambo mengine Wilaya yake inajivunia historia ya kale kutoka utawala wa kijerumani ambapo kumbukumbu nyingi zipo wilayani hapo. “Ni matumaini yangu kuwa mtakapokuja Kilolo mtafurahia utalii wa ndani na mandari nzuri zakuvutia” alisema Abdallah.
Nae kiongozi wa wajumbe wa wanafunzi kutoka chuo cha Taifa cha ulinzi, Capt. Msafiri Hamisi alipongeza kwa mapokezi mazuri timu yake waliyoyapata wilayani Kilolo. Aidha, aliahidi kufikisha mwaliko kutoka kwa mkuu wa Wilaya ya Kilolo wa kutembelea vivutio vya utalii wilayani Kilolo kwa washiriki wajao wa mafunzo kutoka chuo cha Taifa cha ulinzi kupanga kutembelea wilaya ya Kilolo. Alipongeza juhudi zinazofanywa na serikali wilayani Kilolo za kuwaletea maendeleo wananchi wake. “Tunaiona fursa na maendeleo iliyopo mbele kwa wilaya ya Kilolo” alisema Capt. Hamisi.
Timu ya wanafunzi kutoka chuo cha taifa cha ulinzi ipo mkoani Iringa kwa ziara ya siku tano ikishirikisha raia kutoka Tanzania, Kenya, Burundi na Nigeria.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.