DK MAHIGA AZIKARIBISHA NCHI JIRANI MAONESHO YA UTALII YA KARIBU KUSINI
Na. Frank Leonard
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga amezikaribisha nchi jirani za Zambia, Malawi, Msumbuji na Kongo kushiriki maonesho ya Utalii ya Karibu Kusini yatakayokuwa yakifanyika kila mwaka mjini Iringa baada ya serikali kuutangza mkoa wa Iringa kuwa kitovu cha utalii cha mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Aliyasema hayo jana wakati akifunga maonesho ya mwaka huu yaliyofanyika katika viwanja vya Kichangani mjini Iringa kati ya Septemba 29 na Oktoba 2.
“Ni maonesho yanayohusisha mikoa saba ya Nyanda za Juu Kusini ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi. Muda umefika sasa tuzishirikishe nchi jirani na mikoa hii ili kuyafanya maonesho haya yawe ya kimataifa zaidi,” alisema.
Pamoja na kuzialika nchi hizo jirani, ameahidi kusambaza taarifa maalumu ya vivutio vya utalii vya kusini kwa mawakala mbalimbali wanaotangaza utalii wa Tanzania nje ya nchi.
Akifunga maonesho hayo Balozi Mahiga alisema; “Nimefurahishwa sana kushirikishwa katika maonesho hayo natarajia mwakani nitakuwa pamoja nanyi.”
Awali Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alitoa takwimu zinazoonesha maonesho hayo yaliyofanyika kwa mara ya kwanza mwaka jana yakipata mafanikio zaidi mwaka huu.
Masenza alisema wakati mwaka 2016, washiriki katika maonesho hayo walikuwa 127 ambayo ni sawa na asilimia 42 ya washiriki 300 waliotarajiwa, mwaka huu washiriki wameongezeka hadi 435 sawa na asilimia 87 ya washiriki 500 waliotarajiwa.
Alisema kati ya washiriki hao, washiriki wanne ambao ni wajasiriamali wa viwanda vidogo walitoka nchini Kenya.
Alisema maonesho hayo yalijumuisha maeneo sita ambayo ni pamoja na maonesho ya bidhaa za wajasiriamali na watoa huduma za utalii, kongamano la utalii endelevu, usiku wa Utalii kusini, maonesho ya tamaduni na ngoma asilia, maonesho ya wanyama hai na ziara za kutembelea vivutio mbalimbali.
Katika risala yao iliyosomwa na Daimon Mwenda, wajasiriamali wenye viwanda vidogo walitaja changamoto wanazokumbuna nazo katika kuboresha shughuli zao za uzalishaji.
Changamoto hizo ni pamoja ukosefu wa baadhi ya malighafi ambazo hazizalishwi nchini, mlolongo wa kupata vibali na leseni za uanzishwaji viwanda, mitaji, ushindani na bidhaa toka nje na gharama za ununuzi wa mashine za kodi (EFDs).
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.