Mamia ya wakaazi wa Mkoa wa Iringa Wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Peter Serukamba Leo September 21, 2024 wameshuhudia tukio la kihistoria la utiaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara ya lami yenye Km. 104 kutoka Iringa Mjini hadi Hifadhi ya Taifa ya Ruaha
Barabara hiyo ya Iringa- Msembe itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami ikiwa ni mchakato uliochukua takribani miaka 60 hadi utekelezaji wake.
Hafla ya utiaji saini kwa mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo baina ya Wakala wa Barabara Tanzania(TANROADS) na kampuni ya China Henan International Company Limited (CHICO) imefanyika katika uwanja wa Samora, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Ujenzi Mhe.Innocent Bashungwa (Mb) amesema kuwa mkataba wa ujenzi wa barabara ni mafanikio makubwa kwa Tanzania hasa katika kuinua sekta ya utalii na Uchumi Mkoani Iringa.
Aidha Mhe.Bashungwa amewahikikishia wananchi wanaodai fidia ya kupisha ujenzi wa barabara hiyo kuwa watalipwa stahiki zao kwa wakati baada ya tathimini kumalizika.
Akitoa maelezo ya barabara hiyo Mtendaji mkuu wa TANROADS Eng. Mohamed Besta amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa Kilometer 104 utachukua miezi 24 ikigharimu kiasi cha shilingi bilioni 142.56
Akitoa salaamu za Mkoa Mhe. Serukamba ametoa shukrani kwa Serikali huku akiiomba Wizara hiyo kushughulikia kwa haraka suala la fidia.
Kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo kumepongezwa na wabunge wa Mkoa wa Iringa waliohudhuria katika hafla hiyo akiwemo Mhe. William Lukuvi (Isimani), Mhe. Jesca Msambatavangu (Iringa mjini), Mhe. Jackson Kiswaga (Kalenga) na wabunge wa viti maalum Mhe. Nancy Nyalusi na Mhe. Rose Tweve ambao wametaja kama historia kwa mkoa huo na kusema kuwa Serikali imelipa deni kubwa kwa wananchi wa Iringa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.