Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Walmashauri ya Wilaya ya Iringa inaajiri walimu wa muda mfupi katika mkakati wa kukabiliana na changamoto ya upungufu wa walimu wa sayansi.
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Iringa, Mariam Mlilapi alipokuwa akisoma risala ya utii ya wananchi wa halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa Rais Dkt John Magufuli wakati Mwenge wa uhuru ulipokuwa Tarafa ya Isimani wilayani Iringa.
Mlilapi alisema kuwa halmashauri ya Wilaya ya Iringa ina upungufu wa walimu 145 wa masomo ya sayansi. “Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ina mahitaji ya walimu 381 wa sayansi, waliopo mpaka sasa ni walimu 236 hivyo kuwa na upungufu wa walimu hao 145” alisema Mlilapi. Jitihada zinazofanyika kupunguza changamoto ya walimu wa masomo ya sayansi ni kuajiri walimu wa muda mfupi wa masomo hayo kupitia fedha za fidia ya ada kipengele cha taaluma, aliongeza Mlilapi.
Akiongelea ufuatiliaji na usimamizi wa mifumo ya ithibati na ubora wa elimu, kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Iringa alisema kuwa halmashauri hiyo imekuwa ikifanya ziara katika shule ili kukagua mambo mbalimbali yanayolenga utekelezaji wa sera ya elimu ya taifa. “Ofisi ya mthibiti ubora wa elimu kwa kushirikiana na halmashauri imekuwa ikifuatilia, kusimamia na kuhakikisha ubora wa elimu unaotolewa shuleni unakidhi vigezo vilivyowekwa na serikali, ambapo jumla ya shule za sekondari 15 kati ya 36, shule za msingi 85, kati ya 149 na chuo kimoja cha ualimu zimekaguliwa katika kipindi cha Januari-Mei, 2018” alisema Mlilapi.
Mwenge wa uhuru ukiwa katika halmashauri ya Wilaya ya Iringa umekimbizwa umbali wa Km 218 katika Vijiji saba, Kata saba na Tarafa nne.
Ikumbukwe kuwa halmashauri ya Wilaya ya Iringa ina wakazi 254,032 kwa mujibu wa sense ya mwaka 2012, wanaume wakiwa 123,243 na wanawake 130,789. Tarafa sita, Kata 28, Vijiji 133, Vitongoji 747 na Kaya 60,160.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.