Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Mkoa wa Iringa umejipanga vizuri kuwahudumia wananchi wote watakaojitokeza katika uzinduzi wa kampeni ya furaha yangu itakayozinduliwa tarehe 24 mjini Iringa.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa iringa, amina masenza alipokuwa akiongea na waandishi wa habari wa mkoa wa iringa kuhusu maandalizi ya uzinduzi wa kampeni ya furaha yangu ofisini kwake leo.
Masenza alisema kampeni hiyo inatarajia kuvuta watu wengi kujitokeza kupima. “Kwa kuwa kampeni hii, itavuta Watu wengi, Mkoa umejipanga tayari kuhakikisha vitendanishi na dawa za ARV zipo za kutosha katika kila kituo kinachotoa huduma hiyo, ili kuweza kuwahudumia vizuri na kuwaanzishia dawa watakaogundulika kuwa na maambukizi ya VVU na UKIMWI”. Watoa huduma watakuwepo wa kutosha kuwahudumia wananchi watakaojitokeza katika uzinduzi wa kampeni hiyo, aliongeza.
Ili tuweze kufanikisha suala hili na ukizingatia ukweli kwamba tuna asilimia kubwa za maambukizi ya VVU.
Mkuu wa mkoa alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa Mkoa wa Iringa una asilimia 11.3 ya maambukizi ya virus vya UKIMWI. “Hivyo, ninatoa wito kwenu waandishi wa habari, kuibeba kampeni hii ya Furaha Yangu, ili iweze kufanikiwa kama ilivyokusudiwa. Ni imani yangu kuwa vyombo vya habari vikibeba kampeni hii kama Agenda muhimu itasaidia katika uhamasishaji wanaume, makundi mengine na jamii kwa ujumla kuweza kujitokeza kupima VVU na watakaogundulika kuanza kutumia dawa za kufubaza VVU mapema” alisema masenza. Wataalam wa Ofisi yangu na wadau mbalimbali wa mapambano ya VVU na UKIMWI wapo tayari kuwapa ushirikiano mtakaouhitaji katika kuandaa na kutengeneza vipindi mbalimbali vitakavyohusiana na Kampeni hii, aliongeza.
Alisema kuwa katika uwanja wa uzinduzi Mwembetogwa, kutakuwa na huduma za ushauri nasaha na upimaji, uchangiaji wa Damu, huduma mkoba za tiba na matunzo, elimu ya tohara kinga kwa wanaume, uzazi wa mpango, kifua kikuu, elimu ya lishe, huduma za bima ya Afya.
Ikumbukwe kuwa uzinduzi wa kampeni ya Furaha yangu kitaifa ya kupima na kuanza kutumia dawa za kufubaza makali ya VVU mapema ulifanywa na waziri mkuu, Kassim Majaliwa tarehe 19, Juni, 2018 mkoani Dodoma. Ikiongozwa na kaulimbiu “Furaha Yangu” – Pima, Jitambue, Ishi.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.