Na. Dennis Gondwe, Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-Iringa
Kampeni ya Iringa mpya imelenga kuifanya Serikali iwajibike kwa wananchi wake kwa kuwahakikishia huduma bora.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Ally Hapi alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara yake ya Tarafa kwa Tarafa wilayani Kilolo katika shule ya sekondari ya Ilula jana.
Mhe Hapi alisema “dhumuni kubwa la ziara ya Iringa mpya ni kuifanya Serikali iwajibike kwa wananchi wake, Iringa mpya inalenga kuwafanya watendaji wa Serikali wawajibike kwa wananchi”. Serikali lazima iwe na utaratibu wa kujitathmini. Serikali ambayo haina utaratibu wa kujitathmini inakuwa imekalia uzi mwembamba, aliongeza. Ziara ya Iringa mpya ni kutathmini utendaji wa Serikali kwa wananchi wake. “Wote tumepata nafasi ya kujitathmini na kuona wananchi wanatutazamaje kwenye kazi zinazofanya. Ndugu zangu ziara hii ni kioo cha kutathmini utendaji wa mtu mmoja mmoja” aliongeza Mhe Hapi.
Aidha, alimtaka Mkurugenzi tendaji Wilaya ya Kilolo, kuwasimamia vizuri wakuu wa idara na vitengo ili watekeleze majukumu yao na kuwasimamia watumishi walio chini yao. “Mkurugenzi anaweza kuwa mwalimu au mtu yeyote, kwa kuwa anakuwa na wakuu wa idara wa sekta mbalimbali kama elimu, maji, kilimo, mifugo, afya, maendeleo ya jamii, mkaguzi wa ndani akiwasimamia vizuri mambo yanaenda vizuri na kero za wananchi zitaisha. Serikali ni wakuu wa idara, serikali ni wakuu wa vitengo” alisema Mhe Hapi.
Akiwa ziara ya Tarafa kwa Tarafa wilayani Kilolo, Mkuu wa Mkoa alitembea umbali wa Kilometa 943, kufanya mikutano mikubwa mitatu na mikutano midogo 10.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.