Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Mkoa wa Iringa umekagua miradi 18 ya maendeleo yenye zaidi ya shilingi bilioni tatu katika sekta mbalimbali ili kijiridhisha na thamani ya fedha katika utekelezaji wa dhana ya utawala bora.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akisoma taarifa ya mkoa wa Iringa wakati wa kupokea Mwenge wa uhuru kutoka Mkoa wa Mbeya leo.
Masenza alisema kuwa Mkoa kupitia taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) imekagua miradi 18 ya maendeleo katika sekta za maji, elimu na barabara. Miradi hiyo ilikuwa na thamani ya shilingi 3,380,725,980.72. Alisema kuwa lengo la ukaguzi huo ni kufuatilia matumizi na thamani ya fedha katika miradi hiyo. Zimefanyika kazi 12 katika kudhibiti mianya ya rushwa kwa kuchambua mifumo sita na kufanya warsha sita na wadau wa mapambano ya rushwa alisema Masenza.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU Mkoa wa Iringa imetoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa na madhara yake kwa wananchi 4,909 kupitia semina 52, mikutano ya hadhara 25, klabu za wapinga rushwa 63. Aidha, machapisho 1,259 yenye ujumbe wa mapambano dhidi ya rushwa yamegawiwa kwa wananchi.
Akiongelea watuhumiwa wa makossa ya rushwa waliofikishwa mahakamani, mkuu wa Mkoa alisema kuwa watuhumiwa wa makosa ya rushwa kwa kesi nne na majalada 13 ya uchunguzi yakikamilika baada ya kupokea malalamiko 126 ya rushwa. Uchunguzi wa malalamiko mengine unaendelea alisema.
Mkuu wa Mkoa alisema kuwa mapambano dhidi ya rushwa yatawezekana ikiwa kaulimbiu ya mapambano hayo isemayo ‘kataa rushwa-jenga tanzania’ itatekelezwa kwa vitendo.
Mwenge wa uhuru mkoani Iringa utakimbizwa katika Wilaya tatu na halmashauri tano ukikagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi 40 ya maendeleo.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.