IRINGA YARIDHISHWA NA USHIRIKIANO WA WANAHABARI
Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Serikali mkoani Iringa imeridhishwa na ushirikiano inaopata kutoka kwa wanahabari katika kufanikisha mipango ya maendeleo ya mkoa kwa wananchi wake.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya sherehe za siku ya wafanyakazi kitaifa mkoani Iringa jana.
Masenza alisema kuwa waandishi wa habari wamekuwa wakitoa ushirikiano mkubwa kwa serikali ya mkoa katika kufanikisha mipango ya maendeleo. Alisema kuwa ushirikiano wa waandishi wa habari umekuwa chachu ya mafanikio katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika mkoa wa Iringa.
Akiongelea maadhimisho ya siku ya wafanyakazi kitaifa kwa mkoa wa Iringa, Masenza alisema kuwa wakazi wa mkoa wa Iringa wanabahati. “Wanairinga tujihesabu kutambuliwa na kupewa heshima kubwa sana hivyo, tumejisikia vizuri kwa heshima hii tuliyopewa”. Aidha, aliwataka wananchi kutumia sherehe za Mei Mosi kama fursa ya kibiashara. Alisema kuwa watumie nafasi hiyo kuonesha ukarimu kwa wageni watakaotembelea mkoa huo kwa ajili ya kushiriki sherehe hizo.
Wakati huohuo, katibu mkuu wa TUCTA taifa, Dkt Yahya Msigwa aliupongeza mkoa wa Iringa kwa kukubali kuwa mwenyeji wa sherehe hizo. “Sisi kama TUCTA tumerithishwa na ushirikiano unaotolewa na uongozi wa mkoa katika kufanikisha sherehe za Mei Mosi” alisema Dkt Msigwa. Aliseongeza kuwa katika maadhimisho hayo, makongamano ya wafanyakazi yameandaliwa ili kujadili masuala ya kazi na changamoto zinazowakabili wafanya kazi. “Wafanyakazi wanapopewa elimu juu na masuala yanayohusu haki zao migogoro ya wafanyakazi imekuwa ikipungua na ufanisi wa kazi kuongezeka” alisema Dkt. Msigwa.
Maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Mei Mosi mwaka 2018 yataongozwa na kaulimbiu isemayo uunganishaji wa mifumo ya hifadhi ya jamii ulenge kuboresha mafao ya mfanyakazi na yatahudhuriwa na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.