Na. Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji -Mufindi
Jumla ya Miradi 06 yenye thamani ya shilingi bilioni 9.199 imezinduliwa, kuwekewa mawe ya msingi pamoja na kukaguliwa na Mwenge wa Uhuru, ulipokimbizwa katika Halmshauri ya Wilaya ya Mufindi, huku wakimbiza Mwenge kitaifa wakiridhishwa na viwango vya miradi husika na kutanabaisha kuwa vinaendana na thamani ya fedha zilizotumika.
Ukiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi katika ujenzi wa vyumba vya Madarasa Sekondari ya Igombavanu, umezindua klabu ya wapinga rushwa katika Shule ya Sekondari Igombavanu, ujenzi wa zahanati ya Kijiji pamoja na kukagua mradi wa hifadhi ya mazingira katika msitu wa kupandwa wa Halmashauri Kijiji cha Mtili, umezindua ujenzi wa Barabara ya lami Kitiru- Itulituli yenye urefu wa Kilomita 14.972, na mradi wa kilimo na mifugo wa mwananchi kata ya Igowole.
Akizungumza wakati wa kutoa ujumbe wa Mwenge,kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Ndugu. Charles Francis Kabeho, amewahamasisha wananchi kuwekeza katika elimu kwa kugharamia mahitaji muhimu ya Watoto wao, kama mavazi, viatu, Madaftari sanjari na kuchangia mchango wa Chakula cha mchana kwa wanafunzi wa kutwa chini ya ujumbe mkuu wa mbio za Mwenge 2018 “ELimu ni Ufunguo wa Maisha Wekeza Sasa kwa Maendeleo ya Taifa letu”
Aidha, ameendelea Kuhamasisha kuhusu mapambano dhidi ya rushwa, VVU/UKIMWI, dawa za kulevya na mapambano dhidi ya Malaria.
“Maambukizi ya UKIMWI yameendelea kuwa tatizo kubwa katika Mkoa wa Iringa, mkiongozwa na Mkoa wa Njombe wenye asilimia 11.4, wakati ninyi mnashika nafasi ya pili kitaifa kwa kuwa na maambukizi ya asilimia 11.3 hivyo, inatupasa tuchukue hatua za kubadili tabia kwani hali hii ikiendelea hivi ni hatari kwa maendeleo ya Taifa’’ alisema Kabeho
Kwa Upande Wake Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mhe. Jamhuri William, Kupitia risala ya utii kwa mkuu wa nchi, amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwamba, Wilaya yake, itaendelea kutekeleza Maagizo mbalimbali ya Serikali ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa viwanda, usimamizi wa Mbolea ya ruzuku, kuokoa mifumo ya kiikolojia ya bonde la Mto Ruaha mkuu pamoja na suala la Waalimu Kutojihusisha na michango ya Wazazi Shuleni .
Mkesha wa Mwenge wa Uhuru uliambatana na zoezi la upimaji wa maambukizi ya virusi vya UKIMWI na katika upimaji huo, jumla ya watu 435 walijitokeza kujua Afya zao, kati yao wanaume ni 232 na Wanawake ni 203 ambapo katika zoezi hilo ni watu 04 tu ndio waligundulika kuwa na maabukizi ikiwa ni Wanawake 02 na Wanaume 02.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.