MKOA WA IRINGA WAFANYA MAANDAMANO YA KUMPONGEZA JPM
Na. Mwandishi Maalum, Iringa
Wananchi wa mkoa wa Iringa wamefanya maandamano makubwa ya amani ya kumpongeza Rais Dk John Magufuli kwa kuimarisha uchumi na kulinda rasilimali za Taifa.
Katika maelezo ya maandamano ya amani ya wananchi wa mkoa wa Iringa yaliyotolewa na mratibu wa maandamano hayo, Paschal Mhongole katika uwanja wa Mwembetogwa leo asubuhi alisema kuwa wananchi wameamua kuandamana ili kumuonesha Rais Dk Magufuli kuwa wanamuunga mkono katika kuimarisha uchumi na kulinda rasilimali za Tanzania.
Mhongole alisema kuwa baada ya Rais Dk Magufuli kupokea taarifa mbili za kamati za kuchunguza makinikia, yalianza kutolewa maombi kutoka kwa wananchi na makundi mbalimbali juu ya umuhimu wa kufanya maandamano ya amani ya kumuunga mkono Rais Dk Magufuli. “Hivyo wazee waliamua kwenda kumuona mkuu wa mkoa ili kumuomba wananchi kufanya maandamano hayo” alisema Mhongole.
Katika salamu za mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema “katika Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020, inasema kuwa CCM itazielekeza serikali zake kuondoa umasikini, kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa na kusimamia amani, ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao”. Alitoa wito kwa wananchi wote kuungana pamoja kumuunga mkono Rais Dk Magufuli ili Mungu aendelee kumlinda na kumpa nguvu na ujasili katika mapambano yake ya kuwakomboa wanyonge wa Tanzania.
Aidha, aliwataka wananchi kufanya kazi kwa bidii. “Kwa wale walio katika ofisi timizeni wajibu wenu. Kwa wale mlio katika sekta binafsi timizeni wajibu wenu ili wote kwa pamoja tukuze uchumi na kuzalisha malighafi zitakazotumika katika viwanda” alisisitiza Masenza.
Katika maoni ya Maria Sangana, mkazi wa Manispaa ya Iringa kuhusiana na utendaji kazi wa Rais Dk Magufuli, alisema kuwa Rais Dk Magufuli ni mchapa kazi hodari na ni chachu kwa watumishi wengine na wananchi kwa ujumla kuinga utendaji wake ili kukuza uchumi wa Tanzania. “Hata ukiangalia tu muitikio wa wananchi katika maandamano haya ni mzuri. Hii inaashiria kuwa wananchi wengi wanamuunga mkono Rais wetu. Hata ukiangalia ujumbe ulioandikwa katika mabango unasadifu imani waadamanaji waliyonayo kwa Rais” alisisitiza Sangana.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.