Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Makamu wa Rais wa Tanzania, mama Samia Suluhu Hassan amesikitishwa na watu wanaokwamisha juhudi za wananchi kujiletea maendeleo na kuuagiza uongozi wa Mkoa wa Iringa kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.
Mama Hassan alionesha masikitiko yake jana alipokuwa akihutubia mamia ya wananchi wa mji mdogo wa Ilula na vitongoji vyake jana.
Mama Hassan alisema kuwa wapo watu wanaopita mitaani kudumaza kasi ya maendeleo na nguvu za wananchi zinazowekwa katika kujiletea maendeleo. Aliongeza kuwa wapo wafanyabiashara na sekta binafsi wameonesha nguvu zao katika kuunga mkono juhudu za wananchi kuwaletea maendeleo lakini wanakwamishwa na baadhi ya watu kutofikia dhamira ya serikali. “Watu hao wanaodumaza juhudi za maendeleo wanajiita watanzania. Naomba sana kama kuna watu wa aina hiyo, washughulikieni. Sheria, kanuni na miongozo ipo. Hapana hatuwezi kuendelea kwa namna hiyo” alisema mama Hassan.
Akitoa salamu za Rais Dr. John Magufuli, Makamu wa Rais alisema kuwa “Mheshimiwa Rais anawapongeza wananchi wa Kilolo kwa juhudi wanazozifanya kujiletea maendeleo. Anaelewa juhudi mnazozifanya katika kujenga hospitali ya wilaya na hatua mliyofikia. Anaipongeza wilaya kwa kupata hati safi ya hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha 2015/2016” alisema mama Hassan.
Makamu wa Rais aliwataka wananchi wa Kilolo kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Dr. Magufuli na serikali yake ya awamu ya tano kwa kufanya kazi kwa bidii ili maendeleo yaende kwa kasi. Serikali itasukuma sekta za elimu, afya, maji, umeme vijijini na miundombinu ili huduma hizo ziwe rahisi kwa wananchi na kuwaongezea kasi ya kufanya kazi.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.