Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imetakiwa kuviimarisha vikundi vya hiari vya wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini kupitia TASAF ili viwe imara na kufikia sifa za kukopesheka hatimae kuondokana na umasikini.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipofanya ziara maalum ya kuwatembelea wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini katika mtaa wa Ngelewala uliopo Kata ya Mwangata Manispaa ya Iringa leo.
Masenza alisema “Manispaa kiingizeni kukundi cha Amani TASAF Mawelewele kwenye vikundi vinavyokopesheka ili wanufaike na asilimia 5 ya vikundi vya kina mama. Ni vizuri na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotoa misaada kwa vikundi yakaanza na vikundi hivi vya hiari ili viondokane na umasikini”. Aliwakumbusha kuwa wanapokopeshwa fedha lazima kulipa ili nawengine waweze kunufaika na fedha hizo. Aliongeza kuwa umoja ni nguvu siku zote kwa watu wanyonge.
Akiongelea mafanikio ya vikundi kwa wanufaika wa TASAF awamu ya tatu, mratibu wa TASAF Manispaa ya Iringa, Lucy Mtafi alisema kuwa wanufaika wamefanikiwa kuanzisha vikundi. “Uanzishaji wa vikundi vya kuweka na kukopa vya wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF awamu ya tatu umeanza, na wameanza kukopeshana ili kukuza mitaji yao” alisema Mtafi.
Akiongelea changamoto zinazoukabili mpango huo, alizitaja kuwa ni baadhi ya wanufaika kutofuatilia mahudhurio ya maendeleo ya wanafunzi shuleni. Nyingine ni baadhi ya wanufaika kuhama makazi bila kutoa taarifa na akusababisha fedha zao za ruzuku kurudishwa makao makuu ya TASAF.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.