Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Serikali mkoani Iringa imewataka wafanyabiashara wote kulipa kodi kwa mujibu wa sheria ili serikali iweze kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akisalimia wachimbaji wadogo wa mgodi wa nyakavangala katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Nyakavangala kilichopo wilayani Iringa alipokuwa akiongea na wachimbaji wadogo wakati wa ziara ya naibu waziri wa Madini, Dotto Biteko mkoani Iringa jana.
Masenza alisema “katika Mkoa wangu, siruhusu mtu yeyote kufanya biashara bila kulipa kodi. Lazima kulipa kodi. Kodi ndiyo inajenga zahanati, kodi ndiyo inajenga shule na miundombinu yote na kodi ndiyo inalipa mishahara”. Alisema kuwa utamaduni wa kulipa kodi ndiyo utawezesha ujenzi wa barabara ya kuelekea katika machimbo ya Nyakavangala kwa kiwango kinachoridhisha.
Aidha, pamoja na kuwapa pole wachimbaji wa dhahabu wa Nyakavangala kufuatia vifo vilivyotokana na ajali zilizotokea siku za nyuma katika mgodi huo, aliwataka kuzingatia kanuni za usalama. “Sitaki vifo katika Mkoa wangu. Lazima kanuni za usalama zizingatiwe wakati wa uchimbaji wa dhahabu”. Alisema kuwa ushauri wa wakaguzi wa madini uzingatiwe ili machimbo ya Nyakavangala yawe eneo salama kwa wachimbaji wadogo mkoani Iringa.
Wakati huohuo, mkuu wa Mkoa wa Iringa alimuagiza mkuu wa Wilaya hiyo kwenda kuwasikiliza wananchi waliojaribu kubeba mabango katika ziara ya naibu waziri wa Madini ili kufahamu hoja zao na kuzitafutia ufumbuzi.
Akiongea katika majumuisho ya ziara yake yaliyofanyika katika ofisi ya mkuu wa Mkoa, naibu waziri wa Madini, Dotto Biteko alisema kuwa nchi imempata kiongozi anayethubutu kuhakikisha madini yanawanufaisha watanzania. “Rais, Dr John Magufuli ana dhamira ya dhati kuyafanya madini yawanufaishe wananchi wa Tanzania na kuchangia katika pato la taifa. Dhamira yake ni kuona madini yanawanufaisha wachimbaji wadogo na hatimae kufikia hatua ya uchimbaji mkubwa” alisema Biteko.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.