Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Ally Hapi ametoa mwezi mmoja kwa mtu yeyote aliyechukua mashine za kukatia Almasi aisalimishe ofisini kwake.
Agizo hilo alilitoa alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wa Mkoa wa Iringa waliojitokeza katika uzinduzi wa kampeni ya Iringa mpya katika uwanja wa chuo cha afya ya msingi (COTC) mjini Mafinga leo.
Mhe Hapi alisema kuwa kiwanda cha kukata Almasi kilibinafsishwa kikiwa na mashine ya kukata Almasi. “Sasa hakuna mashine hata moja. Majengo yamenunuliwa na serikali kuwa ya Mahakama. Natoa mwezi mmoja kwa yeyote mwenye mashine hiyo aje kuisalimisha ofisi ya mkuu wa Mkoa. Naviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza jambo hilo na kuniletea taarifa” alisema Mhe Hapi.
Akiongelea mapato ya serikali, mkuu wa Mkoa aliziagiza mamlaka za serikali za mitaa kubuni vyanzo vipya vya mapato na kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya serikali. Ukusanyaji mzuri wa mapato ya serikali ndiyo unasaidia katika kuleta maendeleo ya nchi, aliongeza.
Uzinduzi wa kampeni ya iringa mpya utafuatiwa na ziara ya tarafa kwa tarafa itakayofanyika katika tarafa zote 15 za mkoa wa iringa kusikiliza kero za wananchi na kutembelea, kukagua miradi ya maendeleo na kuweka mawe ya msingi.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.