Akifungua kikao hicho Mheshimiwa Hapi amesema, vikao kama hivi vya kukutana na Wadau wa Elimu ni muhimu sana. Hapa tutajua changamoto na mafanikio mbalimbali yaliyopo katika Sekta ya Elimu.
Malengo ya kufanya kikao ni kutathimini hali ya maendeleo ya elimu, kuainisha mafanikio na changamoto za Sekta ya Elimu, mbinu na mikakati ya kutatua changamoto zinazoikabili Sekta ya Elimu, amesema Mheshimiwa Hapi.
Pia kupima fursa za Watendaji wote wa Sekta ya Elimu, kufanya mipango Mkoa huu uwe juu kielimu. Jukumu la msingi ni kuangalia watoto na changamoto zao.
Ameongeza kusema kuwa, hiki kikao ni muhimu sana kwetu na inatakiwa kikae mara mbili kwa mwaka na siyo mara moja kama ilivyozoeleka.
Mheshimiwa Hapi amewapongeza Mkuu wa Wilaya ya Mufindi na Watendaji wake katika Halmashauri za Mufindi na Mafinga Mji kwa kusimamia vema ujenzi wa madarasa na kufanya wanafunzi wote walichaguliwa kuingia Kidato cha Kwanza, kuanza shule kwa wakati. Kisha amewasisitiza Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Iringa Manispaa na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kuharakisha vyumba vya madarasa ili watoto waliofaulu kuanza kidato cha kwanza, kwani katika Halmashauri hizo ina jumla ya wanafunzi 3,480 wamekosa kupangiwa kuanza kidato cha kwanza kwa ajili ya upungufu wa madarasa.
Mheshimiwa Hapi amesema, hakutakuwa na likizo kwa Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Idara ya Elimu na Wakuu wa Shule ambao katika maeneo yao bado kuna changamoto za upungufu wa vyumba vya madarasa, ili wafanye kazi usiku na mchana kuhakikisha wanakamilisha ujenzi huo.
Amemaliza kwa kusema kuwa, kila shule ya msingi na sekondari kuwepo na mlezi wa wanafunzi ambaye atakuwa rafiki, mwenye busara, na kuweza kusikiliza matatizo ya watoto. Kwani watoto wengi wanakabilliwa na wimbi la matatizo ya ubakaji, kulawitiwa na unyanyasaji wa kijinsia na kingono lakini hawana mahali pa kusema matatizo wanayokabiliana nayo. Ameagiza ndani ya mwezi mmoja kila Mkuu wa Shule awe ameleta mapendekezo ya mlezi kwa Afisa Elimu Mkoa. Dawati la Jinsia na Ustawi wa Jamii washirikiane kutoa semina kwa walezi hawa ili wawe na uelewa wa jinsi ya kukabiliana na matatizo ya wanafunzi.
Imetolewa na Ofisi ya Habari Mkoa,
Humphrey Kisika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.