Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,
Michezo mahala pa kazi itumike kujenga na kuimarisha afya za wafanyakazi ili waendelee kutoa huduma nzuri kwa wananchi nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake ya uzinduzi wa michezo ya Mei Mosi kitaifa mwaka 2018 iliyofanyika katika uwanja wa michezo wa Samora mjini Iringa na kusomwa na afisa elimu mkoa wa Iringa, Mwl Majuto Njanga.
Masenza alisema kuwa michezo mahala pa kazi ni muhimu sana katika kusaidia kujenga na kuimarisha afya za wafanyakazi. Alisema kuwa afya za wafanyakazi zinapoimarika zinawawezesha kutoa huduma bora kwa wananchi pamoja na kuongeza tija mahala pa kazi. “Mfanyakazi legelege hatoweza kuzalisha tija au kutoa huduma bora iliyotukuka kwa sababu ya mwili wake kudumaa kwa kukosa mazoezi” alisema Masenza. Aliongeza kuwa michezo mahala pa kazi husaidia kujenga mahusiano mema miongozi mwa wafanyakazi.
Mkuu wa mkoa alisikitishwa na kupungua kwa timu shiriki katika mashindano ya Mei Mosi, 2018 ambapo timu zimepungua kutoka 15 hadi kufikia timu 10. “Nawalaumu sana viongozi wote ambao wameingia woga na kuwanyima fursa wanamichezo wafanyakazi kuja kushiriki kwenye michezo hii ya Mei Mosi kitaifa ambayo mhe Rais ndiye mgeni rasmi katika maonesho haya”.
Aidha, alitoa rai kwa viongozi kuhakikisha michezo inafanyika mahala pa kazi na timu hizo zishiriki katika michezo ya Mei Mosi kitaifa ikiwepo michezo ya SHIMIWI, SHIMMUTA, SHIMISEMITA na BAMMATA. Aliitaka TUCTA kufikisha taarifa kwa menejimenti za timu mbalimbali ili zishiriki kwenye michezo ya Mei Mosi kitaifa.
Akiongelea kaulimbiu ya michezo ya Mei Mosi mwaka 2018 inayosema “Tanzania ya viwanda swadaktaa…kwa ukuzaji wa ajira sambamba na uhamasishaji wa michezo kazini”, kaimu makamu mwenyekiti wa kamati ya michezo ya Mei Mosi taifa, Joyce Benjamin alisema kuwa wanaimani kubwa kuwezekana kwa Tanzania ya viwanda nchini. Alisema kuwa Tanzania ya viwanda itakwenda sambamba na ukuzaji wa ajira na uhamasishaji wa michezo mahala pa kazi.
Akiongelea kupungua kwa timu za michezo kutoka 15 mwaka 2017 hadi kufikia 10 mwaka huu, Benjamin alisema kuwa wadau wote wakae chini na kutafakari swala hilo kama ni woga au ukosefu wa fedha. “Niseme wazi mhe. Mkuu wa mkoa kwamba mhe. Rais, hajakataza michezo. Hatujasikia akikataza michezo hata siku moja…inawezekana wanamuogopa tu yeye kutumia fedha…lakini kwa nini wamuogope…anachotaka mhe Rais ni uhalisia tu wa matumizi kwenye eneo fulani na si vinginevyo” alisema Benjamin.
Michezo ya Mei Mosi mwaka 2018 imeshirikisha timu kutoka Ikulu, Wizara ya Uchukuzi, MUHAS, Hifadhi ya Ngorongoro, Geita Gold Mine, TRA, TANESCO, TTPL-Morogoro, Ukaguzi na RAS Iringa.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.