Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa- Iringa
Wadau wa maendeleo mkoani Iringa wametakiwa kushirikiana katika utekelezaji wa lengo la uanzishaji wa viwanda 100 ili kukuza uchumi wa wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua kikao cha mrejesho wa kampeni ya “Mkoa wetu, viwanda vyetu” pamoja na maandalizi ya maonesho ya utalii karibu kusini kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo jana.
Masenza alisema “katika kutekeleza azma hii ya serikali ya uchumi wa viwanda, tumepewa mwaka mmoja kuhakikisha Mkoa wetu unaanzisha viwanda si chini ya viwanda 100. Hayo ni malengo, lakini utekelezaji wake unategemea sana wadau wote kwa pamoja tunavyoshirikiana kukamilisha agizo hili la serikali”. Aidha, aliwataka wadau wote kutumia fursa hiyo ya uanzishaji viwanda kujikomboa kiuchumi na wananchi kwa ujumla wake.
Katika utekelezaji wa lengo hilo, alisema taasisi nyingine zimewekewa malengo ya utekelezaji. Alizitaja taasisi hizo kuwa ni SIDO Mkoa wa Iringa kujenga viwanda visivyopungua 20. Aliongeza kuwa taasisi kama madhahebu ya dini na vyama vya ushirika pia vimeonesha nia ya kujenga viwanda mkoani Iringa.
Kikao cha kupokea mrejesho wa kampeni ya Mkoa wetu viwanda vyetu kililenga kupokea utekelezaji kwa kuonesha mafanikio na changamoto katika utekelezaji huo.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.