Akitoa ufafanuzi katika mgogoro huo Mkurugenzi wa Halmashari ya Wilaya ya Mufindi Ndugu Netho Ndilito amesema, baada ya kufanya tathimini tuliwaita mara kadhaa kwa barua wadau hawa wa chai ili waje tuzungumze mezani na tukubaliane lakini hawakutaka kuja. Sisi kama Halmashauri tuliamua kuwapeleka Mahakamani. Lakini kabla ya kwenda huko tukaomba Mkuu wa Mkoa atukutanishe na tupate suruhu ya jambo hilli.
Katika kufafanua zaidi chanzo cha mgogoro huo Msaidizi wa Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Ndugu Method Msokele amesema, tuliona tathmini yetu kuwa hakuna malipo ya ushuru kutoka kwa Wadau wa Chai na kwamba Kampuni hizi za Chai hazijawahi kulipa ushuru wa chai wa kiasi cha 3% wa mapato yao ya chai. Kwa mujibu wa sheria kifungu VII (b) wadau wanatakiwa kulipa ushuru kwa Halmashauri, kwani imeonesha kuwa Kampuni ya Uniliver inadaiwa zaidi ya Bilioni 82, Mufindi Tea Company (MTC) inadaiwa zaidi ya Bilioni 30 na Kampuni ya Kiganga (Kisigo Factory) inadaiwa zaidi ya Milioni 993 za Kitanzania.
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mheshimiwa Jamhuri David amesema, sisi na wawekezaji tunafanya kazi kwa ukaribu sana kwani wameajiri watu wengi ambao wanajipatia kipato. Linapojitokeza tatizo kama hili huwa tunachukulia uzito sana, sasa kwa vile leo Mkuu wetu wa Mkoa upo hapa umetukutanisha nadhani jambo hili litafikia muafaka.
Mkuu wa Idara ya Fedha kutoka Uniliver Ndugu Rayson Raja amekiri kuwa na mvutano kati yao, hivyo ameomba wakubaliane na Halmashauri na kuondoka katika mgogoro huo.
Meneja wa MTC Ndugu Mohamed Kasila naye amekiri kuwa na mvutano huo na kuomba kupitia meza ya makubaliano kufikia muafaka wa jambo hili. Kwani fedha wanazodaiwa ni nyingi mno hawataweza kuzilipa.
Mwakilishi wa Bodi ya Chai Ndugu Junis Mwano amesema ukumu la Bodi ya Chai ni kutunza kumbukumbu za kila Kampuni na tunazichakata kila mwezi. Pia amesema Halmashauri zina uwezo wa kutengeneza sheria ndogo za ulipaji ushuru na ipelekwe kwa Wadau ili wazipitie kabla hazijaanza kutumika.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa baada ya kusikiliza pande zote mbili kwa utulivu kabisa alimaliza kwa kusema, mimi kama Mkuu wa Mkoa kazi yangu kubwa ni kusimamia Sheira na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika pande zote mbili kuna hoja ambazo zinakinzana. Hivyo basi nalazimika kuunda kamati ndogo maalum ambayo itakaa mezani wachakate taarifa zote ili tupate ukweli wa jambo hili. Sitapenda kusikia kuwa pande Fulani imekataa kukaa na kuzungumza, naomba mzungumze kwa kufuata sheria na taratibu bila upendeleo wala mahaba wala chuki. Nitatoa muda maalumu wa kamati hii kushughulikia jambo hili, baada ya hapo nitakaa na kamati yangu kushauriana nini kifanyike.
Rai yangu ni kuwa nidhamu ya kukutana na heshima iwepo, kila kampuni itajua waoe watu gani (wataalamu), kwa sababu wote tunatambua umuhimu wa Sekta ya chai. Pia Bodi ya Chai lazima muwepo katika mazungumzo haya.
Nawapongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kwa na nia ya kukusanya mapato, pia Sekta Chai kuonesha nia ya kufanya mazungumzo haya ili tufikie muafaka.
Imetolewa na Ofisi ya Habari,
Mkoa wa Iringa,
Humphrey Kisika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.