Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Watanzania zaidi ya asilimia 50 ya watu wanaoishi na VVU hawajui kuwa wanaishi na VVU mchango mkubwa ukitokana na kiwango cha wanaume kutojitokeza kupima VVU.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua kikao cha maandalizi ya kampeni ya Furaha Yangu, ya kupima VVU na kuanza dawa mapema, kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa.
Masenza alisema “kitaifa inakadiriwa kuwa asilimia 52.2 ya watu wanaoishi na VVU hawajui kuwa wanaishi na VVU. Kwa kiasi kikubwa hali hii inachangiwa na wanaume ambao kiwango chao cha upimaji kiko chini sana, ambacho ni asilimia 45.3 ukilinganisha na kinamama ambao kiwango chao ni asilimia 55.9 kulingana na matokeo ya utafiti wa viashiria vya VVU/UKIMWI (Tanzania HIV Impact Survey 2016/17)”. Umefika wakati kampeni za mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU zielekezwe katika kuwahamasisha wanaume/vijana wa kiume kupima VVU na magonjwa mengine, aliongeza. “Najua jambo hili si jepesi kutokana na hulka za akina baba na mazoea ambayo tayari yameshajengeka katika familia nyingi za kiafrika Tanzania ikiwemo” aliongeza Masenza.
Aidha, alitoa wito kwa akina mama walio katika ngazi za uongozi kuhamasika na kuwahamasisha akina mama wanaowaongoza kuwa na agenda moja ya kuwaunga mkono wanaume na vijana wa kiume kuwa tayari kujitokeza kupima afya zao.
Vilevile, aliwaagiza viongozi ngazi zote mkoani Iringa kutumia kauli mbiu aliyoiongoza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayowalenga wanaume isemayo “Mwanaume Jali Afya Yako, Pima VVU” ili kuweka msisitizo katika ushiriki wa wanaume katika kampeni hiyo.
Uzinduzi wa kitaifa wa kampeni ya “Furaha Yangu” umedhihirisha azma ya Serikali yetu ya awamu ya tano ya kuhakikisha kuwa inaimarisha na kuongeza kasi ya mapambano, ili baada ya kuzifikia hizo “tisini tatu” mwelekeo sasa unabaki ni ule wa kufikia zile “sifuri tatu”; kutokuwepo kwa maambukizi mapya ya VVU, kutokuwepo kwa unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU, na kutokuwepo na vifo vinavyotokana na UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.