KIKOSI KAZI KUNUSURU MTO RUAHA CHARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI AGIZO TOMMY DIARIES FARM
Na Dennis Gondwe, IRINGA
Kikosi kazi namba tatu cha kunusuru ikolojia ya mto Ruaha mkuu kimeridhishwa na utekelezaji wa agizo la kuondoa migomba isiyo rafiki kwa vyanzo vya maji katika shamba la mifugo la Tommy diaries lililopo wilayani Kilolo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na wakili wa serikali mkuu kutoka baraza la Taifa la la hifadhi ya mazingira (NEMC), Benard Kongola baada ya kikosi kazi hicho kwenda kufuatilia utekelezaji wa agizo la tarehe 24/4/2017 lililomtaka muwekezaji huyo kuondoa migomba hiyo shambani kwake wilayani kilolo.
Migomba iliyokatwa.
Kongola alisema “migomba ambayo si rafiki kwa vyanzo vya maji ilikuwa imepandwa ndani ya mita 60 kutoka kingo za mto Ruaha mdogo jambo ambalo ni ukiukwaji wa sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, sehemu ya 57 ibara ndogo ya 1 inayozuia kulima au kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60”. Alisema kuwa walipotembelea shamba hilo kukagua hali ya uhifadhi wa mazingira na ikolojia ya bonde la mto Ruaha mkuu waligundua uharibifu huo wa kimazingira na pamoja na kuwapiga faini ya shilingi milioni 10 kutokana na kulima mahindi na migomba ndani ya hifadhi ya mto na waliwataka kuondoa mazao hayo yaliyolimwa ndani ya mita 60.
Migomba iliyokatwa
Wakili Kongola alizitaka mamlaka za serikali za mitaa kusimamia sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 kwa sababu ipo wazi. Alisema kuwa usimamiaji makini wa sheria hiyo utasaidia kudhibiti shughuli za kibinadamu zinazofanyika ndani ya mita 60 katika nyanzo vya maji jambo linalohatarisha uendelevu wa vyanzo hivyo wilayani Kilolo.
Ikumbukwe kuwa shamba la mifugo la Tommy diaries lilipigwa faini ya shilingi milioni 10 kutokana na kulima mahindi na migomba ndani mita 60 kutoka ukingo wa mto Ruaha. Vilevile, shamba la mifugo la Ndoto pia lilipigwa faini ya shilingi milioni 10 kutokana na kufanya biashara bila kuwa na cheti cha tathmini ya Mazingira (EIA).
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.