Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, IRINGA
Mkuu wa mkoa wa Iringa, Mhe Ally Hapi amezitaka kampuni zote zilizopo mkoani Iringa zinazojishughulisha na ununuzi na uuzaji wa mbao pamoja na uuzaji wa nguzo za umeme kuhakikisha wanalipa kodi ya asilimia tano(5%) kwa mujibu wa sheria za nchi hii.
Ameyazungumza hayo hii leo wakati wa kikao cha wadau mbalimbali alipokuwa akiwasilisha maagizo yaliyotoka kwa waziri mkuu wa serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Kasimu Majaliwa kwenye kikao kilichofanyika jijini Dodoma baada ya kutokea sintofahamu juu ya tatizo la nguzo za umeme.
“Jamani vita ya kupambana na wafanyabiashara wanaokwepa kodi sio jambo rahisi kama ambavyo mnavyofikiri ni vita kubwa kweli kweli na inatisha haswa,hivyo hadi kuona hii leo nimeshinda ujue kuwa serikali ya awamu ya tano haitaki mchezo mchezo kwenye mapato ambayo yanatakiwa kulipwa kwa mujibu wa sheria” alisema Hapi
Wananchi wengi wa Iringa ni maskini wakati wanadhahabu kubwa ya maliasili ya misitu ambayo ndio tegemeo la watanzania kwa asilimia tisini(90) kwa kuwa zao la mbao na nguzo zote zinatoka mkoani Iringa hivyo ni lazima walipe kodi ya asilimia tano ili kuboresha na kuwaondoa wananchi wa mkoa wa iringa kwenye umaskini.
“Hakuna sheria ya kulipa elfu tano kwa nguzo za umeme na mbao bali kuna sheria ya 5% ya kodi ambayo kila mfanyabiashara wa nguzo za umeme anatakiwa kulipa, Hivyo natangaza kuanzia leo wafanyabiashara wote wanatakiwa kulipa hiyo 5% ya kodi ya nguzo za umeme na mbao” alisema Mhe. Hapi
Vilevile mkuu wa mkoa amewaagiza wakurugenzi wote kuhakiki tozo zote za makampuni yanayofanya biashara ya mbao na nguzo za umeme ili kupata mapato yatakayosaidia kuboresha sekta ya Elimu, Afya na kuboresha miundombinu ya wananchi ambao wanachangia kodi kwa maendeleo ya nchi yao.
Serikali ya mkoa wa Iringa haitawavumilia wafanyabiashara wowote wale ambao wanakwepa kodi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi nitawachukulia hatua kali kweli kweli kwa kuwa serikali ya awamu ya tano imewahamasisha wananchi kulipa kodi na wanalipa sasa iweje makampuni ndio yanakwepa kulipa kodi? kwa mkoa huu haitawezekana.
Nawaomba wawekezaji wazawa wa viwanda vya kuchakata mbao na nguzo za umeme kuja kuwekeza mkoani Iringa kwa kuwa bado kuna fursa hiyo na mkoa utahakikisha wawekezaji wazawa wenye sifa wanapata fursa hiyo hata kuiuzia serikali mazao hayo ya mbao na nguzo za umeme.
“Tukiwa na wawekeazji wazawa nina uhakika hawawezi kukwepa kodi maana hakuna sehemu ya kukimbia kwa kuwa hii nchi ni yao lakini pia itachangia ushindani katika soko na kuacha kuitegemea kampuni moja tu ambayo inakwepa kulipa kodi” alisema hayo mkuu wa mkoa Mhe.Hapi.
Mkuu wa mkoa wa Iringa ameitaka kampuni ya uzalishaji na uuzaji wa nguzo za umeme ya New forest, kulipa hilo deni kwa Halmashauri ya Kilolo kiasi cha bilioni 2,970,664,213.82. Pia amezitaka Halmashauri za Mafinga Mji na Mufindi dc kuandaa bili za madai hayo na kisha kuwasilisha kwa kampuni zilizopo katika Halmashauri hizo kwa ajili ya ulipaji wa tozo hizo.
Hata hivyo Mhe. Hapi alisema kuwa kampuni hiyo ya New forest imekuwa ikikwepa kodi tangu mwaka 2007 ilipoanzishwa mpaka sasa ni miaka 12 imekuwa ikisema bado hawajaanza kupata faida kitu ambacho sio kweli. Hivyo amewaagiza TRA na vyombo vya usalama kukagua mali zao zote ili kujua kama kweli hawapati faida.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.