Na. Ofisi ya Mkuu wa mkoa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, mhe Ally Hapi ameiagiza Wilaya ya Mufindi kusimamia ukusanyaji wa mapato ya serikali na kubuni vyanzo vipya vya mapato.
Agizo hilo alilitoa alipokuwa akiongea na wafanyakazi wa Wilaya ya Mufindi katika ukumbi wa CCM Wilaya ya Mufindi katika siku ya pili ya ziara yake ya wilaya kwa wilaya mkoani Iringa.
Mhe Hapi aliitaka Wilaya ya Mufindi kuendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato ya serikali. “Asilimia 78 ya ukusanyaji wa mapato bado ni ndogo. Nataka halmashauri zote za Iringa zisishuke asilimia 90 ya ukusanyaji wa mapato ya serikali. Mamlaka ya mapato Wilaya ya Mufindi ongezeni kasi ya kukusanya mapato ya serikali” alisema mhe Hapi. Katika kusogeza huduma ya ukusanyaji mapato karibu na wananchi, aliwataka wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa kusogeza vituo vya kukusanyia mapato maeneo ya kimkakati karibu na wananchi. Aliwataka kuweka nguvu kwenye kubuni vyanzo vipya vya mapato ili fedha inayokusanywa ipelekwe kwenye huduma za wananchi.
Mkuu wa Mkoa aliziagiza halmashauri za mji Mafinga na Wilaya ya Mufindi kutenga fedha za mikopo ya vijana na akina mama asilimia 10. Alisema kuwa serikali ilishatoa maelekezo kuwa fedha hizo zikopeshwe bila riba na zitolewe zote asilimia 10 ya mapato ya halmashauri. “Katika kukopesha vijana, msikopeshe fedha ghafi, kopesheni mashine za viwanda vidogovidogo” alisema mhe Hapi. Vilevile, aliwataka kuepuka kukopesha vikundi vilevile badala yake kukopesha vikundi vipya.
Akiongelea ujenzi wa viwanda, mkuu wa Mkoa aliitaka Wilaya ya Mufindi kutenga maeneo ya uwekezaji wa viwanda. Alielekeza maeneo hayo yatengwe pamoja na maeneo ya makazi ya wafanyakazi wa viwanda hivyo. “Ili maeneo ya uanzishaji viwanda hivyo yawe na mvuto, mjipange kufikisha huduma za msingi kama maji, umeme, barabara. Watu wa EPZ watafutwe waje walione eneo hilo na kuona namna ya kuliendeleza” alisema mhe Hapi.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa yupo katika ziara ya wilaya kwa wilaya kujitambulisha na kutoa muelekeo wa Iringa mpya anayoitaka katika uongozi wake kwa wafanyakazi.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.