Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-Iringa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Ally Hapi amesikitishwa na matumizi ya ‘force account’ katika ujenzi wa nyumba ya walimu katika Kata ya Mapanda, Tarafa ya Kibengu wilayani Mufindi leo.
Mhe Hapi alisema kuwa baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba moja ya walimu familia sita (6 in one) katika shule ya sekondari Ilogombe, hakuridhika na baadhi ya mambo katika ujenzi huo. “Utaratibu wa matumizi ya ‘force account’ hautekelezwi vizuri. Fedha zinaletwa ili wananchi wanufaike nazo. Nasikitika fundi hatoki kijiji hiki, wala kata hii, wala tarafa hii. Fundi anatoka Mgololo Kata ya Makungu Tarafa ya Kasanga. Hilo siyo lengo la serikali wala ‘force account’. Fundi katumia shilingi milioni 24, lengo ni fedha zibaki katika eneo mradi unapotekelezwa ili wananchi wanufaike nazo” alisema Mhe Hapi.
Mkuu wa Mkoa, aliwapongeza kwa ujenzi wa nyumba moja ya walimu familia sita katika shule ya sekondari Ilogombe na kushauri kuwa vyumba viwe vinajengwa vikubwa zaidi tofauti na vilivyojengwa. Aidha, aliwakumbusha wataalam kuwa siyo lazima fedha zinazoletwa kwa ajili ya ujenzi wa mradi ziishe, zinazobaki zitumike katika miradi mingine ya maendeleo. “Imejengeka tabia ya kuhakikisha fedha zote zinaisha bila kubaki hata kama mradi umekamilika na fedha kubaki, italazimishwa hapo ili fedha zote zionekane zimeisha” alisisitiza Mhe Hapi.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa yupo katika siku yake ya tatu ya ziara ya Tarafa kwa Tarafa akiwa katika Tarafa ya Kibengu amezindua nyumba moja ya walimu ya familia sita katika shule ya sekondari Ilogombe, kukagua ujenzi wa bweni la wanafunzi na miundombinu ya shule ya sekondari Kihansi na kufanya mkutano na wananchi wa Tarafa ya Kibengu.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.