Na. Dennis Gondwe, Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-IRINGA
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Ally Hapi ameshauri mkoa wa Iringa kuangalia uwezekano wa kutumia huduma ya maji kwa njia ya luku ili kuepuka matumizi yasiyo ya lazima ya maji yanayopelekea upotevu wa maji.
Ushauri aliutoa katika mji mdogo wa Ifunda alipotembelea ujenzi wa mradi wa maji wa Ifunda leo.
Mhe Hapi alisema kuwa umefika wakati wa kuanzisha utaratibu wa luku za maji ili mteja alipie huduma ya maji kadri anavyotumia. Utaratibu huo utaondoa tatizo la watu kukwepa kulipia ankara za maji kwa sababu fedha itakuwa inaingia moja kwa moja kwenye mfumo wa malipo. “Ufike wakati mteja anunue maji kabla hajatumia, huo ndiyo uwe muelekeo kwenye mkoa wetu. Hii itasaidia nidhamu katika matumizi ya maji” alisema Mhe Hapi.
Vilevile, aliitaka Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kutoa mafunzo kwa uongozi wa jumuiya ya watumia maji ili waweze kusimamia vizuri mradi huo na kuepuka migogoro katika usimamizi na uendeshaji wake. “Jumuiya hii ipewe mafunzo ya uendesaji wa mradi huu wa maji, usimamizi wa fedha na utunzaji wa kumbukumbu” alisisitiza Mhe Hapi.
Katika taarifa ya ujenzi wa mradi wa maji Ifunda, iliyosomwa na mhandisi wa maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Andrew Kisalo alisema kuwa lengo la mradi huo ni kuboresha huduma ya maji safi baada ya mradi uliokuwepo kuwa na mapungufu katika uzalishaji wa maji na kushindwa kuhudumia wakazi wapatao 5,649 wa kijiji cha Ifunda na Bandabichi. Alisema kuwa mradi huo unagharamiwa na WARIDI kwa shilingi 214,161,642 na mchango wa wananchi shilingi 9,550,000.
Akiongelea changamoto za mradi huo, alizitaja kuwa ni kiwango kidogo cha umeme kutoka katika transfoma iliyopo kuzalisha umeme kwa kuhudumia mradi na jamii kiasi kinachopelekea pampu kushindwa kupampu maji wakati wa mchana na kulazimika kupampu wakati wa usiku kwa nyakati tofauti. Nyingine aliitaja kuwa wateja binafsi waliounganishiwa maji kukaidi zoezi la kuakikiwa upya na kuchukua fomu za kusajili ili kuingia katika utaratibu wa kulipia. Baadhi ya viongozi wa jumuiya ya watumiaji maji kutokumudu kutimiza wajibu wao katika kuusimamia mradi wa maji.
Mradi wa maji wa Ifunda ulibuniwa ili kutekeleza mpango wa kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wa kijiji cha Ifunda na Bandabichi ukiwa ni miongoni mwa miradi ya matokeo ya haraka inayofadhiriwa na wadau wa kimarekani chini ya shirika la WARIDI, ukijengwa na mkandarasi GEK-Girison Investment Co Ltd.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.