Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Wafanyakazi wilayani Mufindi wametakiwa kutoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu yao kila wiki yakionesha jinsi walivyotatua kero za wananchi katika maeneo yao.
Agizo hilo lilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Ally Hapi alipokuwa akiongea na wafanyakazi wa Wilaya ya Mufindi katika ukumbi wa CCM mjini Mafinga leo.
Mhe Hapi alisema kuwa kila wiki mfanyakazi atoe taarifa ya kazi alizofanya na kazi anazotarajia kufanya wiki inayofuata. “Nataka tuwe na mfumo wa utoaji taarifa za utendaji kazi wa serikali kwa wiki, ili tujue nani anafanya kazi na wasiofanya kazi tuwajue. Wakuu wa idara na vitengo mwisho wa siku tutajua matokeo ya utendaji kazi yapoje ili mwisho wa mwezi tupate mishahara kihalali” alisisitiza mhe Hapi. Katika utekelezaji wa agizo hilo, wakurugenzi wa halmashauri ya mji wa Mafinga na Wilaya ya Mufindi waliagizwa kusimamia utekelezaji huo. Aidha, aliwakumbusha wafanyakazi hao kuwa kipimo cha kazi wanazofanya ni utatuzi wa migogoro na kero za wananchi.
Mkuu wa mkoa alisema kuwa anatamani kuona kero za wananchi zinaisha katika mkoa huo. Wafanyakazi wa serikali wanajukumu la kumsaidia mhe Rais kufikia malengo ya nchi. “Kama mhe Rais anafanya ziara mkoani Iringa na anapokelewa na mabango ya malalamiko maana yake wafanyakazi hamumsaidii Mhe Rais. Natamani kuona Mhe Rais anapokelewa kwa mabango yanayopongeza utendaji kazi wake na juhudi zake za kuiletea maendeleo nchi” alisema Mhe Hapi.
Mkuu wa mkoa alisema kuwa anategemea kufanya ziara ya siku 18 ya kutembelea tarafa kwa tarafa. “Nitatembelea miradi ya maendeleo na kufanya mikutano mitatu kwenye kila tarafa. Katika ziara hiyo nitasikiliza kero za wananchi na kila mfanyakazi atajibu kero za wananchi kulingana na eneo lake. Kila mtu atabeba mzigo wake mwenyewe, sitajibu kwa niaba ya mfanyakazi” alisisitiza Mhe Hapi. Aliongeza kuwa kutokana na wafanyakazi kutotimiza majukumu yao, wamekuwa wakizalisha chuki kwa serikali iliyo madarakani kutokana na kushindwa kutatua shida za wananchi. Alisisitiza kuwa hatakuwa tayari kuwavumilia wafanyakazi wanaozalisha chuki na kuifanya serikali ya awamu ya tano ichukiwe na wananchi.
Aliwataka watendaji kuwaheshimu na kuwasikiliza wananchi. “Kumekuwa na tabia ya kuwadharau wananchi na kuwajibu ovyo wanapohitaji huduma katika ofisi zetu. Watendaji ngazi ya vijiji, kata na ngazi zote lazima watenge siku ya kusikiliza kero za wananchi”, alisema.
Mhe Hapi aliwataka wafanyakazi wa serikali kufanya kazi kwa kutenda haki na kutunza siri za serikali. “Wafanyakazi lazima kutenda haki na kuwa waadilifu katika maamuzi yenu. Rushwa na migogoro tujiepushe nayo. Tufanye maamuzi kwa haki kwa maslahi ya wananchi wa Mufindi” alisema mhe Hapi. Aliwakumbusha wafanyakazi hao kuwa kutunza siri za ofisi ni sehemu ya uadilifu.
Mkuu wa mkoa wa Iringa yupo katika siku ya pili ya ziara yake ya kutembelea wilaya za mkoa wa Iringa na kufanya vikao na wafanyakazi na wazee kuelezea dira ya uongozi wake katika falsafa yake ya ujenzi wa Iringa mpya.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.