Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Ally Hapi amezindua kampeni ya Iringa mpya na kuahidi kuiteremsha Serikali kwa wananchi ili kusikiliza na kutatua kero zao.
Mhe Hapi alisema kuwa kampeni ya Iringa mpya inalenga ujenzi na uboreshaji utoaji huduma bora kwa wananchi. “Iringa mpya ni kuiteremsha Serikali chini kwa wananchi kwa kuwatumikia kwa heshima na uadilifu. Nimeamua sitakaa ofisini kusubiri kuletewa taarifa ambazo mara nyingine za uongo, nitawafuata wananchi tarafa kwa tarafa” alisema Mhe Hapi. Aliongeza kuwa atafanya mikutano ya kusikiliza kero za wananchi na watendaji kutoa majibu juu ya kero hizo.
Mkuu wa Mkoa alisema kuwa ziara inalenga kuwakumbusha watumishi wa umma kuwa fedha wanazolipwa lazima wazifanyie kazi kwa kuwahudumia wananchi. “Ziara inalengo la kujenga nidhamu kwenye utumishi wa umma. Lazima watumishi wa umma wajue nafasi walizonazo ni dhamana kwa umma. Tunataka watumishi watakaokutana na changamoto na kuzitatua. Tunataka watumishi wanaojua kuwa rushwa ni adui wa haki. Tunataka watumishi wanaoomba rushwa vyombo vya dola vishughulike nao” alisema Mhe Hapi.
Katika kuhakikisha uwajibikaji kwa watumishi wa umma, Mkuu wa Mkoa aliagiza watumishi wawe wanawasilsiha taarifa ya utendaji kazi za kila wiki na mipango ya utekelezaji wa kazi kwa wiki inayofuata. Kumekuwa na utaratibu wa watumishi wa Serikali kuingia ofisini na kuchati badala ya kufanya kazi, lazima tuweke utaratibu wa kupimana kwa matokeo, alisisitiza.
Uzinduzi wa kampeni ya Iringa mpya utakwenda sambamba na ziara ya kutembelea tarafa kwa tarafa katika Mkoa wa Iringa kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi na watendaji kuzipatia majibu.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.