Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU) mkoa wa Iringa imetakiwa kuhakikisha rushwa inakuwa historia mkoani hapa kwa kushughulikia taarifa za malalamiko ya rushwa kutoka kwa wananchi ili waendelee kuwa na Imani na taasisi hiyo.
Rai hiyo imetolewa na mkurugenzi mkuu wa NSSF Prof Godius Kahyarara alipotembelea banda la TAKUKURU katika maonesho ya shughuli na huduma za wafanyakazi yanayoendelea katika uwanja wa Kichangani mjini Iringa jana.
Prof. Kahyarara alisema kuwa TAKUKURU ina wajibu wa kuhakikisha rushwa inakomeshwa mkoani Iringa ili wananchi waweze watekeleza majukumu yao. Alisema kuwa rushwa imekuwa ikikwamisha maendeleo ya wananchi na kuwanyima haki ya kupata huduma. “TAKUKURU mnawajibu wa kuifanya Iringa kuwa eneo huru dhidi ya rushwa. Na huu ndiyo wajibu wenu wa msingi” alisema Prof. Kahyarara.
Awali afisa muelimishaji wa TAKUKURU mkoa wa Iringa, Aneth Mwakatobe alieleza kuwa hali ya rushwa mkoani Iringa imeendelea kushuka katika miaka ya hivi karibuni. Alisema kuwa hali ya rushwa imeendelea kushuka mkoani hapa kutokana na uelewa wa wananchi kuwa mkubwa. “TAKUKURU mkoa wa Iringa imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi kuhusiana na jinsi ya kukabiliana na rushwa. Katika kuonesha uelewa mkubwa kwa wananchi, wananchi wameendelea kutoa taarifa kwetu na kusaidia uchunguzi kufanyika na kutoa matokea chanya” alisema Mwakatobe.
Afisa huyo aliyataja maeneo yanayolalamikiwa kuwa na vitendo vingi vya rushwa ni yale ambayo watoa huduma wake wanakutana na wananchi moja kwa moja. Alitolea mfano wa maeneo hayo kuwa ni halmashauri, polisi, mahakama, ardhi, na afya.
TAKUKURU ni moja ya waoneshaji wa huduma katika mabanda ya maonesho ya Mei Mosi kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya kichangani mjini Iringa yakitangulia sherehe ya Mei Mosi kitaifa itakayohudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.