WALIOKUWA WAKITUMIA BARABARA YA KM 60 WAPATA YA KM 20
SERIKALI ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan imesikia kilio cha wananchi wa kata ya Udekwa wilayani Kilolo mkoani Iringa ambao kwa miaka mingi waliomba bila mafanikio kujengewa barabara inayounganisha kijiji chao na cha Mahenge.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga alisema ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa Kilometa 20 utawanufaisha wananchi wa kijiji hicho kusafiri na kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi kwenda kijiji cha Mahenge kilichopo barabara kuu ya Iringa, Dar es Salaam.
Alisema kwa miaka yote wananchi wa kata hiyo wamekuwa wakilazimika kusafiri kwa kupitia barabara ya Udekwa, Ilula yenye urefu wa zaidi ya kilometa 60 ili kufika katika kijiji cha Mahenge
Mkuu wa Mkoa alitoa taarifa hiyo juzi kwa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa inayotembelea halmashauri zote za mkoa wa Iringa kukagua utekelezaji wa Ilani na ahadi za maendeleo zilizotolewa na chama hicho kwa wananchi..
“Tunaipongeza serikali ya awamu ya sita, hakika imesikia kilio cha wananchi wanyonge wa Udekwa. Badala ya kusafiri kwa zaidi ya kilometa 60 kufika Mahenge, sasa tutasafiri kilometa 20 tu. Ujenzi wa barabara hii umetupunguzia umbali wa safari kwa zaidi ya kilometa 40,” alisema mkazi wa kijiji hicho, Adriano Mahenge.
Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura)) wa wilaya ya Kilolo, Mhandisi Nkanda Kidola alisema mpaka sasa ujenzi wa barabara hiyo unaendelea vizuri ukiwa umefikia asilimia 70 ya ujenzi wake .
Mhandisi Kidola alisema hadi kukamilika kwake barabara hiyo inayojengwa kwa kiwango cha changarawe kwa kupitia fedha za tozo ya mafuta, itagharimu Sh Milioni 500.
“Barabara hii pia inaweza kutumika kama njia ya mchepuko endapo barabara ya Mahenge, Kitonga hadi Ilula itakuwa na dharula. Magari yanayokwenda Dar es Salaam na Iringa Mjini yanaweza kutumia barabara hii kuepuka dharula hiyo na kuendelea na safari,” alisema.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Dk Abel Nyamahanga ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati hiyo ya siasa alimpongeza Rais akisema ahadi zake za kutumia tozo mbalimbali zilizobuniwa na serikali kutekeleza miradi mbalimbali zimeanza kuleta tija.
“Ni jambo la kujivunia sana kuona barabara hii iliyoshindikana kujengwa kwa miaka mingi na moja ya sababu yake ikiwa ni ufinyu wa bajeti, sasa inajengwa tena kwa fedha zetu wenyewe,” alisema.
Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Justin Nyamoga, aliishukuru serikali kwa kutatua changamoto ya barabara hiyo akisema itachochea zaidi shughuli za kiuchumi zinazofanywa na wananchi wa Udekwa na wilaya ya Kilolo kwa ujumla wake.
Alisema sehemu kubwa ya kata ya Udekwa inapitiwa na hifadhi ya Taifa ya Udzungwa na hifadhi ya mazingira ya asili Kilombero hivyo kujengwa kwa barabara hiyo kutawavutia watalii wengi na hatimaye kukuza pato la wananchi, kata, wilaya, mkoa na Taifa kwa ujumla.
Pamoja na kukagua ujenzi wa barabara hiyo, kamati hiyo ya siasa imetembelea miradi ya madarasa yaliyojengwa kwa fedha za mkopo uliotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) hivikaribuni, kituo cha afya Ilula na miundombinu ya maji Image.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.