TAARIFA YA KATIBU TAWALA WA MKOA KWA UMMA KUHUSU UCHAGUZI WA WANAFUNZI WATAKAOINGIA KIDATO CHA KWANZA 2020 AWAMU YA PILI TAREHE 03/01/2020.
Ndugu
Waandishi wa habari,
Awali ya yote napenda nichukue nafasi hii kuwashukuru wote kwa kuweza kuhudhuria kikao hiki kifupi ambacho ni muhimu kwa Mkoa wetu. Aidha niwape heri ya mwaka mpya 2020.
Ndugu Wanahabari,
Mtakumbuka kuwa tarehe 14/12/2019 niliwasilisha taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza 2020 ambapo nilieleza kuwa Mwaka 2019 Mkoa wa Iringa ulikuwa na jumla ya watahiniwa 25,325 waliosajiliwa kufanya mtihani wakiwemo wavulana 11,900 na wasichana 13,425 katika shule 493, Kati yao watahiniwa 24,998 (wavulana 11,705 na wasichana 13,293) sawa asilimia 98.7 walifanya mtihani. Watahiniwa 22,130 (wavulana 10,324 wasichana 11,806) sawa na asilimia 88.53 walifaulu mtihani huo. Kiwango hiki cha ufaulu kiliongezeka kwa asilimia 5.3 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka uliopita ambapo ufaulu ulikuwa ni asilimia 83.23
Mkoa wetu ulishika nafasi ya tatu (3) kitaifa kati ya mikoa 26 ya Tanzania bara.
Ndugu wanahabari,
Ongezeko la ufaulu lilibua changamoto ya uhitaji mkubwa wa vyumba vya madarasa katika shule zetu za sekondari au ujenzi wa shule mpya za Sekondari ili kuweza kuwachukua wanafunzi wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza. Hali iliyosababisha wanafunzi 3480 (Iringa Manispaa-893, Iringa DC-661 na Kilolo-1926) kushindwa kupangwa kujiunga na Kidato cha Kwanza 2020 kutokana na ukosefu wa vyumba vya Madarasa.
Ndugu wanahabari,
Kutokana na changamoto hiyo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri ziliweka mikakati ya kukabiliana na hali hiyo ili kuhakikisha wanafunzi wote wanajiunga Kidato cha Kwanza kwa wakati. Miongoni mwa mikakati hiyo ni kukamilisha na kupata vibali vya uanzishaji wa shule za sekondari mpya ambapo jumla ya shule tatu za sekondari zimepata vibali ambazo ni Mivinjeni iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na Shule Mbili za Makifu na Izazi zilizopo katika Halmashauri ya Iringa.
Mkakati Mwingine ni upatikanaji wa nafasi wazi katika shule za Sekondari kwa kutumia vyumba vilivyokuwa vikitumika kwa shughuli nyinginezo na pia kuweza kuomba kibali cha kutumia utaratibu wa wanafunzi kusoma kwa awamu mbili kwa siku (Double Shift)
Ndugu Wanahabari,
Sasa, napenda kuchukua nafasi hii kutamka rasmi kuwa wanafunzi wote 3480 (Iringa Manispaa-893, Iringa DC-661 na Kilolo-1926) waliobaki awamu ya kwanza kutokana na upungufu wa miundombinu ya madarasa wamepangiwa shule ili waanze masomo yao ya kidato cha Kwanza Mwaka 2020 na watapaswa kuripoti katika shule walizochaguliwa ifikapo Jumatatu tarehe 06-01-2020 saa 1.30 asubuhi siku ambayo shule zitakapofunguliwa na kuanza masomo mara moja.
Baada ya maelezo haya mafupi nina imani taarifa hii itawafikia wananchi wote wa Mkoa wa Iringa kwa kupitia vyombo vyenu vya habari.
Ninawashukuru sana kwa kunisikiliza.
LUCAS KAMBELENJE
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa
IRINGA
Imetolewa na:
Ofisi ya Habari Mkoa,
Humphrey Kisika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.