Na. Dennis Gondwe, Iringa
Kanda ya kusini inakabiliwa na changamoto ya miundombinu inayosababisha vivutio vingi vya utalii kutofikika kirahisi na watalii kukosa fursa ya kuona hazina hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan katika hotuba yake wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuimarisha usimamizi wa maliasili na kuendeleza utalii kanda ya kusini mwa Tanzania (REGROW), uzinduzi uliofanyika eneo la Kihesa Kilolo mjini Iringa leo.
Hassan alisema kuwa ukanda wa kusini una vivutio vingi vya utalii ambavyo havifahamiki na kufikika. “Kama mnavyofahamu, kuwa ukanda huu una vivutio vingi vya utalii ila kutokana na changamoto za miundombinu, vivutio hivi havifikiki. Katika ziara yangu mkoani hapa nimeshuhudia changamoto ya miundombinu ya barabara katika baadhi ya maeneo, ila napenda kuwahakikishia kuwa serikali ina dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko katika sekta hii kwa kuhakikisha kuwa tunatanua mtandao wa barabara na pia kuweka mikakati thabiti ya kuendeleza vivutio vya utalii vilivyoko kanda ya kusini ili vichangie kwa ukamilifu ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi” alisema Hassan. Aliongeza kuwa kanda ya kusini imejaaliwa hifadhi ya taifa ya Ruaha, Kitulo, milima ya Udzungwa na pori la akiba la Selous. Mengine ni hifadhi ya misitu ya asilia ya Kilombero, milima Rungwe na mashamba ya miti na maliasili.
“Vivutio vya utalii kanda ya kusini vinajumuisha maeneo ya kihistoria ya Kalenga na isimila (Iringa), kumbukumbu za vita vya Majimaji (Ruvuma), Kimondo cha Mbozi (Songwe) maporomoko ya Kalambo (Rukwa), ziwa Ngozi (Mbeya), fukwe nzuri zilizoko katika ziwa Nyasa, Mtwara na Lindi” alisema Makamu wa Rais. Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kutumia fursa hizo kukuza sekta ya utalii.
Akimkaribisha makamu wa Rais, waziri wa maliasili na utalii, Dr. Hamis Kigwangala alisema kuwa mradi wa kuimarisha usimamizi wa maliasili na kuendeleza utalii kanda ya kusini mwa Tanzania (REGROW), utaboresha miundombinu hafifu ya barabara kwa ajili ya kuyafanya maeneo ya vivutio kufikika kirahisi na kuchochea utalii. Aidha, elimu kwa umma itapewa kipaombele katika etekelezaji wa mradi huo.
Kuhusu mapambano dhidi ya ujangili, waziri wa maliasili na utalii, aliwataka wale wote wanaojihuisisha na ujangili kutafuta kazi nyingine ya kufanya. “Wizara tumejiwekea mkakati wa kupambana na ujangili kufikia asilimia sifuri. Wito kwa majangili watafute kazi nyingine ya kufanya. Tutapambana nao kulia na kushoto, mbele na nyuma mpaka tuwamalize” alisema Dr. Kigwangala.
Katika salamu za mkuu wa mkoa wa Iringa, amina masenza alisema kuwa mkoa wa iringa ulichaguliwa kuwa kitovu cha utalii kwa ukanda wa kusini na wizara ya maliasili na utalii kwa lengo la kukuza sekta hiyo kanda ya kusini. Katika kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa, mkoa huo umeunda kamati ya utalii na mikoa mingine kufanya hivyo alisema. Aliongeza kuwa utalii ni agenda ya kudumu mkoani hapo.
Mradi wa kuimarisha usimamizi wa maliasili na kuendeleza utalii kanda ya kusini mwa Tanzania (REGROW) unalenga kukuza utalii na kipato cha wananchi kwa kuboresha miundombinu, kujenga uwezo katika usimamizi wa maliasili na kuwezesha wananchi wanaozUnguka hifadhi kuzalisha kwa tija.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.