Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Serikali mkoani Iringa imetoa maelekezo kuwa vibali vyote vya ziara za elimu ziwe na mkakati wa kulinda haki za watoto dhidi ya ukatili wa aina yoyote.
Maelekezo hayo yalitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Mwl Amina Masenza katika hotuba yake kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya kusoma ngazi ya mkoa yaliyofanyika katika mji mdogo wa Ilula wilayani Kilolo.
Mwl Masenza aliitaka jamii nzima kuwa na sauti ya watoto kuripoti matukio yanayoashiria unyanyasaji wa watoto wote. “Ninaagiza vibali vyote vya ziara zote za kielimu zinazofanyika katika mkoa wetu ziwe na mkakati maalum wa kulinda haki za watoto na kuhakikisha hakuna ukatili wa aina yoyote unaofanyika kwa watoto wetu, kinyume na hapo kisitolewe kibali cha shughuli hizo” aliagiza Mwl Masenza. Vilevile, alizitaka shule zote zenye vyombo vya usafiri kuhakikisha wanapowarudisha watoto kunakuwa na usimamizi makini ili watoto wakubwa wasipate fursa ya kuwanyanyasa watoto wadogo katika vyombo vya usafiri.
Aidha, mkuu wa Mkoa aliwataka walimu kuzingatia nidhamu, uadilifu na uwajibikaji katika maeneo yao ya kazi. “Walimu mnawajibika kwa wanafunzi, kwa jamii kwenye kazi zenu, kwa mwajiri na taifa kwa ujumla. Wajibu wenu walimu ni kumlea mwanafunzi kiakili, kimwili na kiroho ili awe raia mwema na mzalendo wa nchi yetu” alisisitiza Mwl Masenza. Aliwataka walimu kujiepusha na ulevi, wizi, uasherati, rushwa na ubaguzi katika maeneo ya kazi.
Taarifa ya maadhimisho ya wiki ya kusoma Mkoa wa Iringa iliyowasilishwa na kaimu afisa elimu Mkoa wa Iringa, Mwl Farida Mwasumilwe alisema kuwa mpango wa kukuza stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) umepata mafanikio makubwa mkoani hapa. Alisema mpango huo umefanikiwa kuwapatia mafunzo ya stadi za KKK walimu 3,796 kati ya walimu 5326 sawa na asilimia 71.3. Mafanikio mengine aliyataja kuwa idadi ya wanafunzi wasiojua KKK imeshuka. Mkoa una wanafunzi 34,282 kati ya 38,562 wa darasa la pili wanajua kusoma sawa na asilimia 88.91, wanafunzi 4,279 hawamudu KKK. Uwepo wa vitabu vya ziada na kiada kwa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu, aliongeza Mwl Mwasumilwe. Mafanikio hayo yamechangiwa na juhudi za serikali za kukabiliana na changamoto za wanafunzi kutojua kusoma. Pia uwepo wa wa miradi mikubwa miliwi inayoendesha mafunzo ya KKK katika mkoa ambayo ni LANES na TUSOME PAMOJA.
Maadhimisho ya wili ya kusoma Mkoa wa Iringa yalitanguliwa na maadhimisho hayo katika ngazi za halmashauri kuanzia tarehe 31 Mei, 2018 hadi 6 Juni, 2018.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.