Jamii imetakiwa kuwahamasisha vijana waweze kujikita katika kilimo cha maua ili waweze kutengeneza ajira.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipomtembelea mkulima kijana wa maua kutoka wilaya ya Kilolo katika banda la Halmashauri ya wilaya ya Kilolo katika maonesho ya Nanenane mjini Mbeya.
Masenza alisema “hamasisheni vijana wengi kulima maua kwa sababu ni chanzo kizuri cha ajira. Maua yanapendwa na watu wengi na soko lake ni zuri”. Aliwataka wataalam kufikiria mbinu bora zitakazowafanya vijana wengi kujiingiza katika kilimo cha maua katika mikoa ya nyanda za juu kusini kutokana na kanda hiyo kuwa ya kimkakati kwa kilimo hicho.
Akiongelea umuhimu wa maua katika jamii, mkulima wa maua kijana kutoka wilaya ya kilolo, Reminus Sanga alisema kuwa maua ni ajira ya uhakika kwa vijana. “Kwanza kabisa maua ni ajira kwa sababu yanamuwezesha kijana kupata kipato halali na cha uhakika” alisema Sanga. Faida nyingine aliitaja kuwa maua yanatumika katika kutengenezea marashi mbalimbali. Aliongeza kuwa katika sherehe mbalimbali na misiba maua hutumika kama mapambo.
Maonesho ya shughuli za wakulima Nanenane mwaka 2017 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo, “zalisha kwa tija mazao na bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi kufikia uchumi wa kati”.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.