Wakulima na wajasiriamali watakiwa kuweka utaratibu wa kutunza kumbukumbu za mahesabu ili kubaini faida na hasara inayopatikana katika shughuli zao.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara ya kukagua mabanda alipomuwakilisha mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza.
Ayubu alisema “ni vizuri wakulima na wajasiriamali wakafundishwa jinsi ya kutunza kumbukumbu za mahesabu ya kilimo na uzalishaji ili kufahamu gharama na mwenendo mzima wa kazi wanazofanya. Kufanya hivyo kutamsaidia mkulima na mjasiriamali kujua hali halisi ya kazi anayofanya na kuwawezesha kutoa ushuhuda” alisema Ayubu.
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa aliwataka wakurugenzi kuhakikisha wanawapangia malengo maafisa ugani ili waweze kutoa tija katika shughuli za kilimo na mifugo. “Hakikisheni wataalam hawa mnawapangia malengo yanayopimika na wawe na mpango kazi unaotekelezeka. Utaratibu huu utawawezesha wakulima na wafugaji kuhudumiwa” alisisitiza Ayubu.
Akiongelea uzalishaji katika mashamba ya kuzalisha mitamba ya serikali ya Kitulo na Sao-Hill, Katibu Tawala Mkoa aliyataka mashamba hayo kuongeza uzalishaji wa mitamba ili kukidhi mahitaji ya mitamba katika mikoa ya nyanda za kuu kusini. “Mahitaji ya mitamba ni makubwa kwa mikoa ya nyanda za juu kusini, hivyo soko ni la uhakika. Kinachotakiwa ni kuzalisha mitamba zaidi” Alisisitiza Ayubu. Aidha, aliyakata mashamba hayo kuongeza matumizi ya teknolojia katika uzalishaji wa mitamba.
Maonesho ya shughuli za wakulima Nanenane mwaka 2017 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo, “zalisha kwa tija mazao na bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi kufikia uchumi wa kati”.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.