Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa mkoani Iringa watakakiwa kuandaa mpango mkakati wa kuhifadhi maji na vyanzo vyake ili viwe endelevu.
Agizo hilo lilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya maji kilichofanyika katika kijiji cha Mdabulo wilayani Mufindi leo.
Kufuatia uharibifu wa maji na vyanzo vyake kuendelea katika mamlaka za serikali za mitaa, Masenza aliwaagiza wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa kuandaa na kuwasilisha mpango mkakati wa utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vya maji mkoani Iringa. Alisema kuwa maji ni muhimu kwa maisha ya wananchi hivyo, vyanzo vyake vinatakiwa kulindwa ili viwe endelevu. Vilevile, aliwataka kutumia sheria ya maji katika usimamizi na uhifadhi wa vyanzo vya maji katika maeneo yao.
Aliwataka pia kusimamia mikataba na miradi ya maji ili iwe vizuri. Alisema kuwa usimamizi mzuri wa mikataba ya miradi ya maji utasaidia kupunguza migogoro baina ya wakandarasi na serikali.
Wakati huohuo, mkuu wa mkoa wa Iringa alimtaka mhandisi wa maji wa mkoa kuandaa na kuwasilisha mkakati wa kuanzisha jumuiya za watumia maji katika wilaya zote mkoani Iringa. Alisema kuwa jumuiya za watumia maji zina mchango mkubwa katika usimamizi wa rasirimali maji katika mamlaka za serikali za mitaa.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.