Na. Dennis Gondwe, Afisa Habari, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa- Iringa
Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wilayani Mufindi wametakiwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili iendane na thamani ya fedha zinazotolewa na Serikali.
Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Ally Hapi alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara yake ya Tarafa kwa Tarafa wilayani Mufindi katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi jana.
Mhe Hapi alisema “wakurugenzi simamieni vizuri utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yenu ili kujiridhisha na thamani ya fedha iliyotumika katika utekelezaji wake. Kuna madudu mengi yanafanyika katika miradi ya maendeleo kutokana na watumishi wasio wazalendo”. Vilevile, aliwataka watumishi wa umma na taasisi binafsi kusimamia miradi iliyokusudiwa kutekelezwa kwa kuzingatia falsafa ya Iringa mpya, ili iwe na viwango na maslahi kwa Taifa.
Aidha, aliwataka kusimamia watumishi wanaowaongoza ili wawahudumie wananchi vizuri. “Katika Iringa mpya nataka wananchi wetu wahudumiwe vizuri hasa wananchi wanyonge. Wananchi wanyonge hawana fedha za kwenda mahakamani, wananchi wanyonge hawana fedha za kwenda kwenye mabaraza ya Ardhi wala hawana nauli ya kusafiri kwenda kufuatilia haki zao. Tukiwakwaza hawa hawana mtu wa kumlilia wala kushtaki zaidi ya kusubiri viongozi wawatembelee” alisisitiza Mhe Hapi.
Akiwa wilayani Mufindi, Mkuu wa Mkoa alitembelea Tarafa za Kibengu, Kasanga, Sadani, Malangali na Ifwagi. Pamoja na mambo mengine, alifanya mikutano mikubwa mitano ukiwemo mkutano wa uzinduzi wa kampeni ya Iringa mpya na mikutano midogo midogo 12 na wananchi kupewa fursa ya kuhoji na wataalam kujibu kero za wananchi.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.