Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wanafunzi wanufaika wa mpango wa kunusuku kaya masikini nchini (TASAF) kupitia ruzuku ya elimu wametakiwa kuwashirikisha walimu katika masuala yanayohusu taaluma na ustawi wao ili waweze kufaulu.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akiongea na wanafunzi wanufaika wa TASAF wa shule ya msingi Kitwiru iliyopo Kata ya Kitwiru Manispaa ya Iringa hivi karibuni.
Ayubu alisema “watoto wangu mpo hapa kwa ajili ya kusoma na wote kufaulu, si ndiyo. Walimu wenu wapo hapa kwa ajili ya kuwafundisha na kuwasaidia kufaulu hivyo msiwaogope. Wafuateni kwa ushauri na maelekezo ili muweze kusoma vizuri na wote kufaulu, sawa”. Alisema kuwa serikali inatoa fedha kwa wanafunzi hao kiasi cha shilingi 2,000 kwa mwezi ili waweze kununua mahitaji ya muhimu ya shule. Serikali inataka kuona kila mtoto wa kitanzania anasoma vizuri ili aweze kujitegemea na kuchangia katika kukuza pato la Taifa.
Nae mratibu wa TASAF Mkoa wa Iringa, William kingazi aliwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kuwa wasikivu kwa walimu na wazazi. “Nyie wanafunzi lazima muwe na ndoto kwamba mtakapomaliza masomo mnataka kuwa watu wa aina gani. Ndoto hizo ziwasaidie kusoma kwa bidii ili muweze kuzifikia” alisema Kingazi. Aidha, aliwataka walimu kuwafuatilia wazazi wanufaika wa mpango wa TASAF ili waweze kuwanunulia watoto sare za shule kwa wale ambazo sare zao zimechanika ili wasijione tofauti na wengine.
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa alifanya ziara maalum ya ufuatiliaji kwa wanafunzi wanufaika wa mpango wa TASAF kupitia elimu katika Manispaa ya Iringa kujifunza changamoto zinazowakabili. Katika ziara hiyo aliambatana na mratibu wa TASAF Mkoa, afisa mipango, mhasibu, mkaguzi wa ndani na afisa habari.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.