Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Watanzania wametakiwa kuwaenzi mapacha walioungana Maria na Consolata Mwakikuti kwa kupendana, kusaidiana na kuvumiliana katika kutekeleza majukumu yao.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa elimu, sayansi na teknolojia Prof. Joyce Ndalichako alipoongoza mamia ya wananchi katika mazishi ya mapacha hao kwa niaba ya serikali mkoani Iringa.
Prof. Ndalichako alisema kuwa Maria na Consolata wameacha funzo kubwa kwa watanzania. Mapacha hawa waliishi kwa upendo, kuvumiliana na kushirikiana. Maria na Consolata ni mashujaa. “Watanzania tunatakiwa kuwaenzi mapacha hawa kudumisha upendo, kusaidiana na kushirikiana” alisema Prof. Ndalichako. Aliongeza kuwa somo kubwa waliloliachia taifa ni kujituma katika kazi. Alisema kuwa ulemavu siyo kikwazo katika kutekeleza majukumu, bali ni maumbile tu na kuitaka jamii kutokuwatenga watu wenye ulemavu katika kushiriki shughuli za kijamii na kielimu.
Wakati huohuo, mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema kuwa Maria na Consolata walijitambua, kujiamini na kujikubali. Aliitaka jamii kutokuwaficha watoto wenye ulemavu kwa sababu serikali ya Dkt John Magufuli ipo kwa ajili ya kuwahuhumia. “Serikali itashughulika na wote wanaoficha watoto wenye ulemavu” alisisitiza Masenza. Aidha, aliipongeza kamati ya maandalizi ya mazishi ya Maria na Consolata kwa kazi nzuri.
Maria na Consolata Mwakikuti walizaliwa wilayani Makete mkoani Njombe zaidi ya miaka 21 iliyopita na kupata elimu ya msingi wilayani makete, elimu ya sekondari walipata wilayani Kilolo na elimu ya juu katika chuo kikuu cha kikatoliki cha Ruaha mjini Iringa.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.