ZIARA YA MKUU WA MKOA PAMOJA NA KAMATI YA SIASA MKOA WA IRINGA KUKAGUA MIRADI KATIKA HARMASHAURI YA MANISPAA IRINGA.
WAKAZI wa kata ya Mkimbizi na maeneo jirani mjini Iringa wanatarajia kuanza kupata huduma za afya kupitia kituo cha Afya Mkimbizi, kinachojengwa katika kata hiyo kwa zaidi ya Sh Milioni 250.
Fedha hizo ni sehemu ya makusanyo ya tozo ya miamala ya simu zilizotolewa na serikali kwa halmashauri ya manispaa ya Iringa ili kuwezesha ujenzi wa kituo hicho katika kata hiyo yenye idadi kubwa ya watu, mjini Iringa.
Mbali na kituo hicho, serikali pia imetoa Sh Milioni 12.5 za tozo hizo kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya Sekondari Ipogolo.
Taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mh.Queen Sendiga imepongeza ujenzi wa miradi hiyo iliyoelezwa kwamba itasaidia kusogeza huduma za afya karibu na wananchi na kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani.
Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa ilitembelea miradi hiyo hivikaribuni na kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wake.
Wakati mradi wa ujenzi wa kituo cha afya umefikia asilimia 60, madarasa mawili katika shule ya sekondari Ipogolo yamekamilika na tayari yameanza kutumiwa na wanafunzi wa shule hiyo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Abel Nyamahanga alisema ujenzi wa majengo hayo (kituo cha afya na madarasa) utasaidia sana katika kuboresha huduma katika manispaa hiyo.
“Tunaanza kuona umuhimu wa tozo kila tunapoona miradi kama hii. Tuna kila sababu ya kuunga mkono mipango ya serikali kwani faida zake ni nyingi na muhimu kwa wananchi wote,” alisema.
Wakati huo huo kamati hiyo imeridhishwa pia na ujenzi wa barabara ya Don Bosco Mawelewele- Zizi na Kitasengwa inayojengwa kwa kiwango cha lami.
Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) wa wilaya ya Iringa, Barnabas Jabiry alisema wakati barabara ya Donbosco Mawelewele ina urefu wa kilometa moja ya Kitasengwa ni ya kilometa 0.65.
Mbali na kupendezesha mji, Jabiry alisema miradi hiyo itakapokamilika itapunguza adha ya usafiri kwa wakazi wa kata ya Mwangata, Mkwawa na Isakalilo mjini Iringa.
“Kupitika vizuri kwa barabara hizo kutasababisha wananchi husika kuweza kufanya shughuli zao za kijamii na kiuchumi kwa urahisi,” alisema.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema ujenzi wa machinjio ya kisasa ya Ngelewala umefikia zaidi ya asilimia 90.
Mh.Sendiga amesema“matarajio ya mkoa na manispaa ya Iringa ni kuona kwamba machinjio hiyo inaanza kufanya kazi ifikapo Machi mwaka huu.”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.